
Winga wa Bournemouth, Justin Kluivert, alizua taharuki katika sare ya 0-0 dhidi ya Crystal Palace baada ya kumvua suruali kiungo Ismaila Sarr kwa njia ya kushangaza.
Tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa kipindi cha pili katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza iliyokuwa na mvutano mkubwa katika uwanja wa Selhurst Park. Wote wawili walionywa kwa kadi za njano kutokana na kisa hicho.
Tayari hali ya mchezo ilikuwa ya wasiwasi kufuatia hatua ya refa Samuel Barrott kumtoa mchezaji wa Palace, Chris Richards, kwa kadi ya pili ya njano katika muda wa majeruhi wa kipindi cha kwanza – uamuzi ulioibua utata mkubwa.
Licha ya kipindi cha kwanza kuwa na mchezo wa kawaida bila makabiliano makali, Barrott alikuwa ametoa jumla ya kadi saba za njano kufikia mapumziko.
Dakika moja tu baada ya kipindi cha pili kuanza, mchezo ulilipuka. Kluivert, aliyekuwa amerudi baada ya kukosa mechi tatu kutokana na majeraha, alimchezea faulo beki wa kulia wa Palace, Daniel Muñoz, katika dakika ya 46.
Kluivert alisimama haraka na kujaribu kuendelea na mchezo, lakini Sarr alimzuia huku akiwa amesimama juu yake. Katika hali ya mshangao, Kluivert alimvuta Sarr suruali na kumwacha akiwa na boksa zake nyeusi pekee mbele ya kamera na mashabiki waliostajabika.
Sarr alijibu kwa hasira, akamkabili Kluivert na kisha wote wakaanza kushikana na kusukumana kabla ya wenzao kuwatawanya. Refa Barrott alipuliza kipenga na kuwapatia wote kadi za njano.
Kluivert, mwenye umri wa miaka 25, tayari alikuwa kwenye mvutano katika kipindi cha kwanza baada ya Richards kumuangusha kwa kosa lililomgharimu kadi ya pili ya njano. Hata hivyo, marudio ya tukio hilo yalionyesha kuwa mguso ulikuwa hafifu na Kluivert alionekana kuzidisha maumivu.
Kilichozua zaidi maswali ni kwamba Alex Scott hakutozwa kadi ya pili kwa tukio kama hilo dakika chache kabla ya Richards kutolewa. Badala yake, Barrott alionekana kumpa onyo la mwisho.
Kwa upande wa Palace, huu ulikuwa ni mfululizo wa kadi nyekundu ya tatu kwenye mechi mbili za nyumbani. Katika mechi yao iliyopita, walifanikiwa kushinda 2-1 licha ya Marc Guehi na Jean-Paul van Hecke kutolewa nje.
Hata hivyo, timu ya kocha Oliver Glasner ilifanikiwa kupata pointi moja licha ya drama zote, huku mechi ikimalizika bila bao.