
Leeds United na Burnley wamethibitisha kurejea kwao rasmi katika Ligi Kuu ya England msimu wa 2025/26, baada ya kusajili ushindi muhimu katika michuano ya Championship siku ya Jumatatu.
Leeds walianza siku kwa kishindo, wakiiadhibu Stoke City kwa mabao 6-0 katika uwanja wa nyumbani. Matokeo hayo yaliwaweka kwenye nafasi nzuri ya kurejea ligi kuu, wakisubiri tu Sheffield United wasiposhinda dhidi ya Burnley katika mechi ya jioni. Na walichokitazamia kikatimia — Burnley wakashinda 2-1, na hivyo timu hizo mbili zikapanda moja kwa moja daraja kabla ya msimu kumalizika.
Mabao mawili ya Josh Brownhill yaliwapa Burnley ushindi huo muhimu, huku Joel Piroe akiwaka moto upande wa Leeds kwa kufunga mabao manne ndani ya kipindi cha kwanza pekee. Mholanzi huyo sasa anaongoza kwenye mbio za Kiatu cha Dhahabu cha Championship akiwa na mabao 19, mawili zaidi ya mshambuliaji wa Norwich, Borja Sainz.
Leeds wanarejea ligi kuu baada ya kukosekana kwa misimu miwili, na mafanikio yao yanampa fahari kocha Daniel Farke ambaye amewahi pia kuipandisha Norwich City daraja mara mbili — mwaka 2019 na 2021. Farke pia aliongoza Norwich katika mechi 49 za EPL kabla ya kujiunga na Leeds.
Kwa upande wa Burnley, huu ni ushindi wa kihistoria kwa kocha Scott Parker, ambaye sasa amepandisha timu daraja mara tatu akiwa meneja. Kabla ya mafanikio haya na Burnley, aliifikisha Fulham ligi kuu mwaka 2020 na kisha Bournemouth mwaka 2022.
Kwa sasa, Leeds na Burnley wote wana pointi 94. Kwa kuwa zimesalia mechi mbili pekee na Sheffield United wako na pointi 86, hakuna uwezekano wowote wa kuzidiwa pointi hata wakipoteza mechi zote mbili zilizobaki.
Timu ya Tatu Kupatikana Kupitia Mchujo
Timu ya tatu itakayoungana na Leeds na Burnley kupanda EPL itapatikana kupitia mchujo wa Championship. Klabu zitakazomaliza nafasi ya tatu hadi ya sita zitachuana katika nusu fainali za mikondo miwili kabla ya fainali ya mchujo itakayofanyika Wembley.
Ratiba ya Mchujo (Saa za BST):
Nusu Fainali:
- Mei 8, saa 3 usiku: Nafasi ya sita vs Nafasi ya tatu
- Mei 9, saa 3 usiku: Nafasi ya tano vs Nafasi ya nne
- Mei 12, saa 3 usiku: Nafasi ya tatu vs Nafasi ya sita
- Mei 13, saa 3 usiku: Nafasi ya nne vs Nafasi ya tano
Fainali:
- Mei 24: Mchezo wa mwisho utafanyika Wembley Stadium kuamua timu ya mwisho kupanda EPL.
Hatua Zilizobaki kwa Leeds na Burnley
Leeds na Burnley wataidhinishwa rasmi kama klabu za Ligi Kuu katika Mkutano Mkuu wa EPL utakaoandaliwa kiangazi hiki. Hapo ndipo kila moja itakapopokea cheti rasmi cha uanachama.
Mashabiki wa klabu hizo watajua wapinzani wao wa kwanza wa msimu mpya mnamo Jumatano, Juni 18, saa 4 asubuhi (BST), ratiba kamili ya msimu wa 2025/26 itakapotangazwa. Ligi hiyo itaanza rasmi Ijumaa, Agosti 16.
Kwa sasa, ni furaha ya aina yake kwa wapenzi wa Leeds na Burnley ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu kurejea kwenye jukwaa kubwa la soka la Uingereza.