
Paris St-Germain iliibuka na ushindi mnono dhidi ya Real Madrid na kujikatia tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la Dunia la Klabu la Fifa dhidi ya Chelsea Jumapili.
Mechi hii ya nusu fainali iliyofanyika katika Uwanja wa MetLife ilikamilika kama mashindano ndani ya dakika 24 tu, huku mabingwa wa Ligi ya Mabingwa wakiiangamiza timu hiyo ya Uhispania.
Fabian Ruiz alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya sita baada ya makosa makubwa kutoka kwa beki wa Real, Raul Asencio — huku mwamuzi akiruhusu mchezo kuendelea baada ya Thibaut Courtois kumfanyia faulo Ousmane Dembele.
Winga wa Ufaransa Dembele alikimbia kwa kasi dakika tatu baadaye na kufunga kwa utulivu baada ya Antonio Rudiger kukosa mpira.
Ruiz kisha akafunga bao la tatu baada ya ushirikiano mzuri wa pasi kati ya Achraf Hakimi na Dembele.
Real, ambao walimkosa Trent Alexander-Arnold aliyekuwa majeruhi, hawakutoa upinzani mkubwa, na Goncalo Ramos akaongeza bao la nne mwishoni kwa PSG, akihitimisha maonyesho ya kiwango cha juu.
Mfungaji bora wa muda wote wa PSG, Kylian Mbappe, alikuwa uwanjani kushuhudia maonyesho hayo ya kuvutia kutoka kwa klabu yake ya zamani.
Tangu mshambuliaji huyo wa Ufaransa alipojiunga na Madrid mwaka mmoja uliopita kwa uhamisho wa bure, PSG imekuwa timu bora zaidi kwa kiasi kikubwa na sasa inawania Kombe la Dunia la Klabu kuwa taji lao la nne mwaka 2025 (au la tano ikiwa Kombe la Jamii la Ufaransa litahesabiwa).
Na licha ya Mbappe kuwa na jumla ya mabao na pasi 48 za mabao msimu wa 2024-25 akiwa na Real, wamehitimisha kampeni hiyo bila taji lolote.
Hakuna timu inayoweza kukabiliana na kasi, pasi na mashambulizi ya timu ya Luis Enrique ya PSG, ambayo iliicharaza Inter Milan 5-0 na kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa, pia imeifunga Atletico Madrid 4-0, Bayern Munich 2-0 (wakiwa na wachezaji tisa), na sasa Real Madrid 4-0 katika ardhi ya Marekani.
Ruiz alifunga mara mbili lakini washirika wake wa kiungo walikuwa bora pia. Real hawakuweza kuizuia safu ya ushambuliaji ya PSG, wala Hakimi aliyekuwa beki wa kulia.
Kulikuwa na kwaheri ya hisia kwa Luka Modric mwenye umri wa miaka 39, ambaye alicheza mechi yake ya 597 na ya mwisho kwa Real, na sasa ataelekea AC Milan.
Tangu fainali ya Coupe de France, PSG imeshinda mechi zake tano za hatua ya mtoano katika mashindano yote kwa jumla ya mabao 18-0.
Real Madrid, ambao hawakuwa wamepoteza mechi yoyote ya Kombe la Dunia la Klabu kabla ya hii, walifungwa mabao matatu katika dakika 25 za mwanzo kwa mara ya kwanza tangu 9 Novemba 2003 walipocheza dhidi ya Sevilla kwenye La Liga.
PSG itakutana na Chelsea katika fainali ya Jumapili, itakayofanyika pia huko New Jersey. Watakuwa na mechi mfululizo dhidi ya timu za London, wakianza msimu wa 2025-26 kwa Super Cup ya Uefa dhidi ya Tottenham tarehe 13 Agosti.
Real Madrid hawatarajiwi kucheza tena hadi mechi yao ya kwanza ya La Liga. Kwa sasa, mechi hiyo imepangwa kufanyika nyumbani dhidi ya Osasuna tarehe 19 Agosti, ingawa Real wanajaribu kuahirisha mchezo huo ili kupata muda wa mapumziko zaidi.