Michael Olunga aeleza sababu zake kugura Laliga

Olunga alisema kuwa alipendezwa sana na uwanja wa Santiago Bernabeu wa klabu ya Real Madrid.

Muhtasari

•Akizungumza na Jalang'o kwenye kipindi cha Bonga na Jalas siku ya Jumatano, mshambulizi huyo wa klabu ya Al-Duhail ya Qatari alisema kuwa jambo hilo lilichangiwa na kukosa nafasi za kucheza.

•Reysol walimsajili kwa  shilingi milioni 190 za Kenya, ambayo ni bei ya chini kushinda aliyokuwa amenunuliwa nayo na klabu Guizhou. Thamani yake ilikuwa imeshuka kutoka shilingi milioni 400 za Kenya ambazo Guizhou walitumia kumsajili kutoka Djurgarden ya Uswidi.

Michael Olunga akicheza dhidi ya Barcelona
Michael Olunga akicheza dhidi ya Barcelona
Image: Hisani

Mshambulizi matata wa Harambee Stars, Michael Olunga  amezungumzia sababu zake kuondoka Laliga licha ya sifa tele zinazomiminwa ligi hiyo ya Uhispania.

Olunga ambaye alichezea klabu ya Girona msimu wa 2017/18 amesema kuwa thamani yake kama mchezaji alishuka kwa kipindi ambacho alikuwa huko Uhispania.

Akizungumza na Jalang'o kwenye kipindi cha Bonga na Jalas siku ya Jumatano, mshambulizi huyo wa klabu ya Al-Duhail ya Qatari alisema kuwa jambo hilo lilichangiwa na kukosa nafasi za kucheza.

"Mchezaji yeyote anataka kucheza kila wiki. Hiyo ndiyo inafanya thamani yako kama mchezaji kuenda juu. Unavyocheza zaidi ndivyo unavyoweza kupata uzoefu zaidi, watu wanaweza kukuona, unapata kujua mengi na kiwango cha mchezo wako kinapanda" Olunga alisema.

Mchezaji huyo ambaye aliwahi kuchezea Tusker, Thika United na Gor Mahia za Kenya alisema kuwa alihusishwa kwenye mechi 14 pekee kati ya 38 zinazochezwa msimu wote na alianzishwa kwenye mechi tatu tu kati ya hizo.

Kwa wakati huo, Olunga alikuwa amesajiliwa na klabu ya Girona kwa mkopo kutoka klabu ya Guizhou ya China.

Kukosa kucheza kwake hakukumridhisha Olunga ingawa alisema kuwa ilikuwa nafasi kubwa kwake. Alisema kuwa hali ya kukosa kucheza ilichangia thamani yake kushuka.

"Nikiwa pale nilikuwa nacheza vizuri ingawa sikuwa nacheza mara kwa mara. Thamani yangu ilianguka kwani vile nilkosa kuchezeshwa hakuna mtu angeniona. Skauti hawezi kuja kukutazama ukiwa huchezi. Lazima akutambue ukicheza" Olunga alieleza.

Kipindi cha mkopo  katika timu ya Girona kilipoisha mwaka wa 2018, Olunga alirudi kwa klabu yake nchini China kwani timu hiyo ya Uhispania haikuwa na nia ya kumnunua.

Aliporudi Uchina alipata hali sio ya kupendeza kwani tayari kulikuwa na wachezaji watano raia wa kigeni. Hapo akaamua kujiunga na Kashiwa Reysol ya Ujapani ambao walimhakikishia kuwa atakuwa anapata nafasi ya kucheza.

"Waliponihakikishia kuwa nitacheza angalau 75% ya mechi zote niliamua kujiunga nao" Alisema Olunga.

Reysol walimsajili kwa  shilingi milioni 190 za Kenya, ambayo ni bei ya chini kushinda aliyokuwa amenunuliwa nayo na klabu Guizhou. Thamani yake ilikuwa imeshuka kutoka shilingi milioni 400 za Kenya ambazo Guizhou walitumia kumsajili kutoka Djurgarden ya Uswidi.

Olunga alibobea sana kwenye klabu ya Reysol kwa kipindi cha miaka miwili ambayo alikaa pale na akapendwa sana na mashabiki wa klabu hiyo.

Hata hivyo, Olunga alikiri kuwa alipendezwa na mtindo wa kandanda uliokuwa unachezwa Uhispania na akasema akapa nafasi ya kurudi pale hawezi sita.

"Vile nilikuwa Uhispania niliweza kuona mpira wa kandanda kwa mtazamo tofauti. Hata kama sikucheza sana, nilifurahia uzoefu ambao nilipata . Niliichukulia kama nafasi kubwa ambayo nikaipata tena katika hali nzuri zaidi inaweza kuwa nzuri sana. Hata kama nimecheza kwenye ligi hiyo, ni kama ile chakula tamu ambayo ukikula unataka kurudia tena" Olunga alisema.

Olunga alisema kuwa alipendezwa sana na uwanja wa Santiago Bernabeu wa klabu ya Real Madrid.