Ulimwengu wa soka sasa umeingia katika kipindi cha mapumziko ya kimataifa huku mechi za raundi ya saba katika ligi ya Premier zikichezwa wikendi ambayo imepita.
Klabu 20 za EPL zilijitosa kwenye nyanja mbalimbali nchini Uingereza kila mmoja akitazamia kuboresha nafasi ya kunyakua taji hilo.
Mechi ya ufunguzi ili kuwa kati ya washindi wa EPL mara 13 Manchester United na Everton ambayo ilichezwa mida ya saa nane alasiri siku ya Jumamosi.
Baada ya kupimana nguvu kwa kipindi cha dakika 90 katika uga wa Old Trafford, kila mmoja aliondoka na pointi moja moja baada ya mechi hiyo kuishia sare ya 1-1. Mabao ya mshambulizi Antony Martial na kiungo wa Everton Andros Townsend ndiyo yalipatia timu hizo alama mojamoja.
Mechi nne zaidi zilichezwa Jumamosi mida ya saa kumi na moja jioni ambapo washindi wa Champion League msimu uliopita Chelsea walipata ushindi mkubwa wa 3-1 dhidi ya wageni wao Southampton na kusonga kileleni mwa jedwali. Mechi hiyo ilikuwa ilikuwa sare ya 1-1 hadi dakika ya 77 ambapo kiungo James Ward-Prowse alionyeshwa kadi nyekundu na hapo nguvu za Southampton zikafifia na wakaongezewa mabao mengine mawili.
Wolves waliangamiza wageni wao Newcastle kwa mabao 2-1 huku Leeds wakipata ushindi wa 1-0 dhidi ya wageni wao Watford. Mechi kati ya Burnley na Norwich iliishia sare ya 0-0.
Mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ilikuwa kati ya Brighton na Arsenal ambayo ilichezwa mida ya saa moja unusu. Hakuna bao lolote ambalo lilishuhudiwa katika dakika 90 za mchuano huo.
Mechi zingine nne zilichezwa siku ya Jumamosi ambapo timu sita ziliingia uwanjani mida ya saa kumi alasiri.
Tottenham waliweza kuwazima wageni wao Aston Villa kwa mabao 2-1, West Ham wakaumizwa nyumbani na Brentford kwa mabao 1-2 huku mechi kati ya Crystal Palace na Leicester ikiisha ikiwa sare ya 2-2.
Mechi kubwa zaidi ya wikendi ilikuwa kati ya washindi wa EPL 2020/21 Manchester City na washindi wa EPL 2019/20 Liverpool. Kila mmoja alijinyakulia pointi moja moja kwenye mchuano huo ambao ulichezewa ugani Anfield mida ya saa kumi na mbili unusu jioni baada ya mechi kuishia sare ya 2-2..
Washambulizi Sadio Mane na Mo Salah walifungia Liverpool huku klabu ya Pep Guardiola ikifungiwa na Phil Foden na Kevin De Bruyne.
Kwa sasa Chelsea inaongoza kwenye jedwali na pointi 16 huku Liverpool, Manchester City na United zikifuata na pointi 15, 14, 14 mtawalia. Burnley, Newcastle na Norwich zinakalia nafasi tatu za mwisho na pointi 3, 3, 1 mtawalia.