Mshambuliaji wa Gabon, Pierre Emerick Aubameyang ni mchezaji mmoja mweney furaha kubwa baada ya kufanikiwa kusaini mkataba na miamba wa London, Chelsea katika siku ya mwisho kabisa ya uhamisho akitokea Barcelona.
Aubameyang ambaye awali alikuwa anachezea Arsenal kabla ya kuhamia Nou Camp alionekana akicheza na familia yake huku wote wakiwa wamevalia jezi ya Chelsea.
Video hiyo iliyovujishwa kwenye mtandao wa Twitter inamuonesha Aubameyang akiwa ameshikilia jezi yake nambari 9 ya Chelsea huku akicheza kwa furaha pamoja na familia yake yote.
Watu kadhaa wanaonekana wakiungana naye kwa densi huku wote wamevalia jezi hiyo na wanamitandao wanahisi kabisa hii ni familia yake.
Mchezaji huyo ambaye wengi wanamjua kuwa na mapenzi ya dhati kwa klabu yake ya awali Arsenal wanasubiri kuona jinsi ambavyo ataichezea Chelsea na kulimaliza tatizo la safu ya ufungaji mabao katika timu hiyo.
Inasemekana Aubameyang ana tattoo ya timu ya Arsenal na hilo ndio wengi wanahisi mapenzi yake bado yako pale licha ya kuondoka kwa njia ya kishari mwaka mmoja uliopita.
Mpaka sasa, mchezaji huyo ameisakatia Chelsea mechi mbili chini ya makocha wawili tofauti na angali bado kufunga bao, ila wengi wanahisi anahitaji muda zaidi ili kupona kutokana na jeraha alilolipata usoni ambalo linamfanya kucheza na ukigo usoni.