Michuano ya mwisho ya hatua ya makundi za Kombe la Dunia zilichezwa Ijumaa jioni katika jiji la Doha, nchini Qatar.
Jumla ya mechi nne zilichezwa siku ya Ijumaa ambapo timu nne zilifuzu kuingia raundi ya mwondoano huku timu zingine nne zikikusanya virago vyao na kuelekea nyumbani baada ya kubanduliwa nje.
Ghana na Cameroon za Afrika, Serbia ya Ulaya na Uruguay ya Amerika Kusini ni timu ambazo zilitimuliwa kutoka kwa kombe hilo siku ya Ijumaa huku Ureno,Korea Kusini Uswizi na Brazil zikifuzu kusonga mbele.
Brazil iliweza kumaliza katika kilele cha kundi G licha ya kupoteza 0-1 dhidi ya Cameroon. Switzerland ilichukua nafasi ya pili ya kundi hilo baada ya kuilaza Serbia 3-2.
Hapo awali Ureno ilichukua uongozi wa kundi H licha ya kupigwa 2-1 na Korea Kusini ambayo ilichukua nafasi ya pili. Licha ya Uruguay kuipiga Ghana 2-0 haikuweza kufuzu kuingia raundi ya muondoano huku ikichukua nafasi ya tatu nayo Ghana ikishika mkia.
Ghana, Cameroon, Serbia na Uruguay ziliungana na timu zingine kumi na mbili katika safari ya kurudi nyumbani ya mapema. Timu kumi na mbili ambazo zilitimuliwa hapo awali ni pamoja na Qatar, Ujerumani, Ubelgiji, Costa Rica, Saudi Arabia, Mexico, Tunisia, Denmark, Iran, Wales, Ecuador na Canada.
Timu zilizosalia zitamenyana kati ya Jumamosi ,Desemba 3, na Jumanne Disemba 6 ili kubaini watakaofuzu kuingia robo fainali.
Hii hapa ratiba ya Michuano hiyo:
Disemba 3:
Uholanzi vs Marekani - 6PM
Argentina vs Australia- 10PM
Disemba 4:
Ufaransa vs Poland - 6PM
Uingereza vs Senegal - 10PM
Disemba 5:
Japan vs Croatia - 6PM
Brazil vs Korea Kusini - 10 PM
Disemba 6:
Morocco vs Uhispania- 6PM
Ureno vs Uswizi - 10pm