logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mihangaiko ya kupata kocha bora yapelekea Chelsea kumteua tena Frank Lampard

Lampard alifutwa kazi na Chelsea mwezi Januari 2021 kufuatia matokeo hafifu.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri06 April 2023 - 03:51

Muhtasari


•Lampard anaripotiwa kukubali mkataba wa muda mfupi wa kuwa meneja wa muda wa The Blues hadi mwishoni mwa msimu.

•The Blues walimtimua kocha mkuu Graham Potter siku ya Jumapili, takriban miezi saba tu baada ya kujiunga nao.

Lampard aonekana Stamford Bridge

Frank Lampard anatarajiwa kurejea katika kazi ya ukocha wa Chelsea, zaidi ya miaka miwili baada ya kutimuliwa kutoka katika Klabu hiyo ya London.

Raia huyo wa Uingereza anaripotiwa kukubali mkataba wa muda mfupi wa kuwa meneja wa muda wa The Blues hadi mwishoni mwa msimu.

Chelsea imeafikia kumkabidhi mchezaji huyo wake wa zamani kazi hiyo baada ya kumpiga kalamu Graham Potter siku chache zilizopita.

The Blues walimtimua kocha mkuu Graham Potter siku ya Jumapili, takriban miezi saba tu baada ya kujiunga nao. Hii ni kufuatia msururu wa matokeo hafifu ambayo klabu hiyo imekuwa ikiandikisha katika wiki za hivi majuzi.

Katika taarifa yao, Chelsea walitangaza kwamba mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 47 alikubali kuondoka katika klabu hiyo. 

"Graham amekubali kushirikiana na klabu kuwezesha mabadiliko mazuri," taarifa ya klabu hiyo ilisoma.

Potter alijiunga na klabu hiyo ya London mwezi Septemba, mwaka jana baada ya kutimuliwa kwa Mjerumani Thomas Tuchel. Miongoni mwa mafanikio yake machache ni kwamba ameiwezesha klabu hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini kwa upande mwingine ameiacha katika nafasi ya 11 kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza zikiwa zimesalia takriban mechi 10 tu.

Klabu hiyo ilimfuta kazi Frank Lampard Januari 2021 baada ya kuwa kocha mkuu kwa miezi 18. Thomas Tuchel alichukua nafasi ya gwiji huyo wa klabu baada ya kushuka kwa matokeo katika miezi michache iliyopita.

Mjerumani huyo hata hivyo hakudumu sana katika Chelsea kwani pia yeye alionyeshwa mlango mwezi Septemba mwaka jana.

Tuchel alibadilishwa na Graham Potter ambaye pia alipigwa kalamu mapema mwezi huu.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved