Klabu ya Paris Saint-Germain almaarufu PSG imeendelea kupoteza wafuasi wa Instagram kwa kasi kubwa sana kufuatia habari za kuondoka kwa mshambulizi matata wa Argentina, Lionel Messi.
Messi ambaye alijiunga na PSG Agosti 2021 anaripotiwa kuchezea klabu hiyo ya Ufaransa mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ilipofungwa 2-3 na Clemort. Mchezaji huyo ambaye anaaminika kuwa miongoni mwa wanasoka bora zaidi kuwahi kutokea duniani aliwavutia mashabiki wengi katika PSG miaka miwili iliyopita.
Ukurasa wa Instagram wa PSG ulikuwa umejizolea wafuasi zaidi ya milioni 71 lakini katika siku chache zilizopita umepoteza zaidi ya wafuasi milioni 2.5. Kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii, ukurasa huo ulikuwa umepungua hadi kufikia wafuasi milioni 68.7.
Watu wengi wamehusisha kupungua kwa wafuasi wa akaunti hiyo ya Instagram na habari za hivi majuzi za kuondoka na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 kufuatia kukamilika kwa msimu wa 2022/23.
Nyota huyo wa Argentina anaripotiwa kulenga kurudi katika klabu yake ya zamani, Barcelona ili kustaafu akiwa pale.
Mwezi uliopita, Rais wa Barcelona Joan Laporta alisema klabu hiyo ni "nyumba" ya Messi huku wakitarajia kumsajili tena fowadi huyo msimu huu wa joto.
Mkataba wa Muargentina huyo katika klabu ya Paris St-Germain unamalizika mwezi huu, huku ripoti zingine zikimhusisha na Saudi Arabia.
Lakini katika mahojiano na shirika la utangazaji la Uhispania TV3, Laporta alisema Barcelona inaweza kushindana na mtu yeyote kuwania saini ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35.
"Historia inatuunga mkono, hisia ni kali sana, tuna mashabiki milioni 400 duniani kote pia," alisema
Messi aliondoka kwa wababe hao wa Catalan miaka miwili iliyopita baada ya miaka 21 katika klabu hiyo lakini amekuwa na wakati mgumu katika misimu yake miwili nchini Ufaransa, huku mashabiki wakimzomea mara kwa mara.