Rasmi Mount ni mali ya Manchester United baada ya kuigura timu yake ya utotoni, Chelsea

Mount amesaini mkataba wa miaka mitano hadi 2028 na chaguo la kuongeza kwa mwaka mwingine mmoja na mashetani wekendu.

Muhtasari

• Mason Mount amekamilisha uhamisho wake wa kutoka Chelsea na kuwa mchezaji wa kwanza wa Erik ten Hag.

• Jumanne, Mason Mount aliwaaga mashabiki wa Chelsea wakati mchezaji huyo wa  England akikaribia kuhamia mahisimu wakubwa wa timu yake ya zamani Manchester United.

Manchester United yadhibitisha usajili wa Mason Mount.
Manchester United yadhibitisha usajili wa Mason Mount.
Image: Manchester United

Timu ya ligi kuu EPL, Manchester United imedhibitisha usajili wa kiungo wa zamani wa Chelsea Mason Mount kwa pauni milioni 55.

Mason Mount amekamilisha uhamisho wake wa kutoka Chelsea na kuwa mchezaji wa kwanza wa Erik ten Hag wakati meneja huyo wa Manchester United akitafuta kuboresha ushindi wa msimu uliopita wa Carabao Cup na kumaliza katika nafasi ya tatu.

Mount amesaini mkataba wa miaka mitano hadi 2028 na chaguo la kuongeza kwa mwaka mwingine mmoja na mashetani wekendu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anaimarisha timu hiyo ya Ten Hag baada ya kufuzu kwa ligi ya mabingwa, huku Mount akipendelea kucheza kama namba 10 anatarajiwa kutoa ushindani kwa Christian Eriksen na Bruno Fernandes. 

"Siwezi kusubiri kuwa sehemu ya klabu hii kushinda mataji makubwa. Kila mtu anaweza kuona kwamba klabu imefanya vyema chini ya Erik ten Hag. Baada ya kukutana na meneja na kujadili mipango yake, nilipata msisimko zaidi kwa misimu ijayo, na niko tayari kwa kazi ngumu inayotarajiwa hapa." Mount alisema.

Jumanne, Mason Mount aliwaaga mashabiki wa Chelsea wakati mchezaji huyo wa  England akikaribia kuhamia mahisimu wakubwa wa timu yake ya zamani Manchester United.

Mount, ambaye alikuwa mhitimu wa akademia ya Chelsea, aliichezea Chelsea kwa takriban miaka 18 kuanzia alipo kuwa na umri wa miaka 6 pekee yake.

"Kutokana na uvumi uliokuwa ukienea mitandaoni katika kipindi cha miezi sita iliyopita, hii inaweza kuwa si jambo la kushangaza kwenu, lakini sio rahisi kusema kwamba nimefanya uamuzi wa kuondoka Chelsea," alisema katika video kwenye Instagram yake.

Manchester United sasa wanaelekeza juhudi zao kwa nafasi ya mlinda lango baada ya mkataba ya golikipa wao wa miaka mingi David Degea kutamatika. Man United sasa wanamlenga mlinda lango wa Inter Milan, Ander Onana ambaye aliisaidia timu hiyo kufika fainali ya ligi ya mabingwa.

Mababe hao wa soka watahitajika kutoa zaidi ya pauni milioni 60 ili kuweza kupata saini yake Onana.