Paul Pogba apigwa marufuku ya muda kwa kosa la matumizi ya dawa za kusisimua misuli

Vipimo viliyofanywa kwa kiungo huyo wa kati wa Juventus vilionyesha viwango vya testosterone.

Muhtasari

•Mwanasoka Paul Pogba amesimamishwa kwa muda kucheza kwa kosa la kutumia dawa za kusisimua misuli.

•Jumatatu jioni, Juventus ilitoa taarifa kuthibitisha taarifa hizo ikisema kiungo huyo amesimamishwa kwa muda.

Paul Pogba
Image: HISANI

Mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Paul Pogba amepigwa marufuku ya muda kucheza soka kwa kosa la kutumia dawa za kusisimua misuli.

Vipimo viliyofanywa kwa kiungo huyo wa kati wa Juventus mwenye umri wa miaka 30 na tume ya kitaifa ya Italia ya kupambana na dawa za kusisimua misuli (Nado) vilionyesha viwango vya testosterone. Testosterone ni homoni ambayo huongeza uvumilivu wa wanariadha.

Pogba alifanyiwa vipimo baada ya klabu yake ya sasa Juventus kushinda 3-0 dhidi ya Udinese mnamo Agosti 20. Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hakutumika wakati wa mechi lakini alichaguliwa kwa uchunguzi wa dawa za kulevya baada ya mechi.

Iwapo atapatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli, anaweza kupigwa marufuku kati ya miaka miwili na minne.

Jumatatu jioni, Juventus ilitoa taarifa kuthibitisha taarifa hizo ikisema kiungo huyo amesimamishwa kwa muda.

"Klabu ya Soka ya Juventus inatangaza kwamba leo, Septemba 11, 2023, mchezaji wa mpira wa miguu Paul Labile Pogba amepokea amri ya tahadhari ya kusimamishwa kutoka kwa Tume ya Kitaifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya kufuatia matokeo ya vipimo vilivyofanywa tarehe 20 Agosti, 2023," ilisema taarifa hiyo.

Nado alisema Pogba alikiuka sheria za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli walipopata dawa iliyopigwa marufuku "metaboli za testosterone zisizo asilia" na matokeo "yaliendana na asili ya nje ya misombo inayolengwa".

 Kiungo huyo wa kati ana siku tatu za kufanya uchambuzi wa kupinga matokeo kwa Nado.