logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Africa Football League: Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini yaiadhibu Petro Atletico ya Angola, 0-2

Mechi mbili zaidi zitachezwa Jumapili jioni katika Nchi mbili tofauti.

image
na Samuel Maina

Michezo22 October 2023 - 05:40

Muhtasari


  • •Mamelodi Sundowns walifurahia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Petro Atletico ya Angola katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Estadio 11 de Novembro.
  • •Mechi mbili zaidi zitachezwa Jumapili jioni katika Nchi mbili tofauti.
  •  
walipata ushindi dhidi ya Petro Atletico Jumamosi jioni

Mechi nyingine ya kusisimua ilichezwa katika siku ya pili ya mashindano mapya ya Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) mnamo siku ya  Jumamosi jioni.

Miamba wa soka wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns walifurahia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Petro Atletico ya Angola katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Estadio 11 de Novembro mjini Luanda, Angola kati ya saa kumi na mbili unusu jioni na saa mbili unusu. 

Kipindi cha kwanza kilimalizika bila bao kutoka upande wowote huku Gilberto wa Petro Atletico akikosa mkwaju wa penalti dakika ya 42.

Alikuwa ni Marcelo Ivan Allenda Bravo wa Mamelodi Sundowns ambaye alitangulia kufunga katika dakika ya 67 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Junior Mendieta.

Zikiwa zimesalia takriban dakika 10 tu za muda wa kawaida, Mamelodi Sundowns waliongeza nafasi zao za ushindi kwa kuongeza bao la pili kupitia kwa kiungo Thapelo Maseko.

Sundowns imekuwa timu ya kwanza kuandikisha ushindi katika Ligi mpya ya Soka Afrika iliyofunguliwa rasmi siku ya Ijumaa. Awali, Simba S.C ya Tanzania na Al Ahly ya Misri zilitoka sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Mechi mbili zaidi zitachezwa Jumapili jioni katika Nchi mbili tofauti.

TP Mazembe ya Congo itaikaribisha Esperance Tunis ya Tunisia kwenye Uwanja wa Stade TP Mazembe saa kumi na mbili kamili jioni.

Enyimba ya Nigeria nao watakuwa wenyeji wa Wydad ya Morocco kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio mjini Uyo saa tatu kamili Jumapili usiku.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved