Ilikuwa ni kipindi cha hisia sana wakati fowadi wa Liverpool Luis Diaz alifunga katika dakika za nyogeza na kusaidia klabu yake kupata angalau pointi moja kutoka kwa mechi yao dhidi ya Luton Town siku ya Jumapili jioni.
Vijana wa Jurgen Kloop walikuwa nyuma kwa bao moja hata baada ya dakika 90 za kawaida kuisha na ilichukua juhudi ya Diaz katika dakika ya 95 kufikisha matokeo kwa sare ya 1-1.
Bao la mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia halikuwa la hisia tu kwa sababu lilisawazisha mchezo lakini pia kwa sababu alitumia nafasi hiyo kuagiza kuachiliwa huru kwa baba yake aliyetekwa nyara. Baada ya kufunga bao, uso wa Diaz hakujawa na tabasamu kubwa kama inavyotokea kwa wafungaji wengi lakini badala yake alivuta shati na kuonyesha maandishi kwenye t-shati aliyokuwa amevaa ndani.
"Uhuru kwa baba!" yalisoma maandishi ya Kihispania kwenye shati la Diaz.
Hata wachezaji wenzake wakishangilia bao hilo lililohitajika, pia walimfariji kwa matatizo ya kisaikolojia anayopitia wakati baba yake akiwa hajulikani alipo.
Wazazi wote wawili wa Díaz walitekwa nyara wakiwa wamenyooshewa bunduki katika mji aliozaliwa wa Barrancas na waasi wa mrengo wa kushoto wa Jeshi la Ukombozi la Kitaifa (ELN) tarehe 28 Oktoba. Maafisa wa usalama walifanikiwa kumuokoa mamake lakini baba yake, Luis Manuel Díaz bado hajulikani aliko.
Baada ya mechi ya Jumapili jioni, staa huyo wa Colombia mwenye umri wa miaka 26 alitoa taarifa kuwafahamisha watekaji nyara uchungu ambao familia yao inapitia kwa sasa.
Pia alitumia fursa hiyo kuomba kuachiliwa kwa mzazi wake huyo na kutaka mashirika ya kimataifa ya usalama kusaidia kumrejesha nyumbani.
"Leo mwanasoka haongei nanyi, leo Lucho Díaz, mtoto wa Luis Manuel Díaz, anazungumza nanyi. Baba yangu ni mfanyakazi asiyechoka, nguzo yetu katika familia na ametekwa nyara. Kila sekunde, kila dakika, uchungu wetu unakua. Mama yangu, kaka zangu na mimi tumekata tamaa, tumefadhaika na hatuna maneno ya kuelezea kile tunachohisi,” Diaz aliandika.
Aliongeza, “Mateso haya yataisha tu tutakapokuwa naye nyumbani. Nawaomba mmuachilie mara moja, mkiheshimu uadilifu wake na mmalize kusubiri kwa uchungu haraka iwezekanavyo. Kwa jina la upendo na huruma, tunaomba mfikirie upya matendo yenu na mturuhusu kupona."