logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ole Gunnar akiri kumrejesha Christiano Man United haukuwa uamuzi sahihi, afichua shida aliyoleta klabuni

Kocha huyo raia wa Norway alikiri kwamba kuwa na Ronaldo kwenye timu yake kuliwakosesha raha wachezaji wengine.

image
na SAMUEL MAINA

Michezo06 March 2024 - 12:28

Muhtasari


  • •Kocha Ole Gunnar Solskjaer amekiri kwamba kumsajili Cristiano Ronaldo mwaka 2021 ulikuwa uamuzi usio sahihi.
  • •Kocha huyo raia wa Norway alikiri kwamba kuwa na Ronaldo kwenye timu yake kuliwakosesha raha wachezaji wengine.

Kocha na mchezaji wa zamani wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amekiri kwamba kumsajili Cristiano Ronaldo mwaka 2021 ulikuwa uamuzi usio sahihi.

Christiano alirejea Old Trafford mwishoni mwa dirisha la uhamisho wa majira ya joto la 2021, huku kukiwa na ripoti kwamba angeweza kujiunga na wapinzani wao Manchester City. Katika kipindi chake cha pili katika United, alifunga mabao 24 katika msimu wake wa kwanza. Timu hiyo hata hivyo ilishindwa kutwaa taji lolote na Solskjaer alitimuliwa takriban miezi mitatu baada ya kumsajili.

Katika mahojiano na podikasti ya Sky Bet's Stick To Football, kocha huyo wa Norway alisema kwamba kusainiwa kwa mshambuliaji huyo wa All Nassr mwenye sifa ya juu ulikuwa uamuzi wa haraka.

“Ulikuwa uamuzi wa haraka sana. Hatukufikiria kwamba Cristiano angepatikana na kwamba angehama,” Ole Gunnar alisema.

Aliongeza, "Ilipodhihirika kwamba anaondoka Juventus, ni wazi kulikuwa na vilabu vingine vilivyomtaka - lakini nilifurahi. [United] iliniuliza, ‘Ungependa tujaribu hili?’. Nilisema ndio - ni wazi tunajua Cristiano ni mchezaji bora, na ana miaka 37."

Licha ya kufanikiwa kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 39, Ole Gunnar alikiri kwamba hatua hiyo haikufanya kazi kwa mchezaji huyo wala klabu hiyo.

"Lakini lazima tusimamie - yeye ndiye mfungaji bora zaidi duniani. Haukufaa kwangu, haukufaa kwa Cristiano, lakini ulikuwa uamuzi sahihi wakati huo."

Kocha huyo raia wa Norway alisema kuwa hana majuto juu ya kumsajili Ronaldo, hata hivyo alikiri kuwa naye kwenye timu yake kuliwakosesha raha wachezaji wengine.

 "Cristiano ni tofauti na Antony Martial ambaye alikuwa mbele, au kama tungecheza na Mason [Greenwood] au Marcus [Rashford] mbele. Edinson Cavani ndiye aliyeumia zaidi Cristiano alipoingia - tulicheza na kumfanya Edinson kuelewa jinsi tulivyocheza," alisema.

Ole Gunnar pia alizungumzia jinsi nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno alitaka kuwekwa benchi baada ya kucheza mechi kadhaa ila aklalamika alipoheshimu ombi lake.

"Cristiano - unapomfahamu na kuzungumza naye, alitaka kucheza michezo mitatu kati ya minne, aligundua kuwa anazeeka pia. Lakini unapomwacha mara moja, hafurahii! Kwa mpira, naye kwenye timu, haikuwa shida. Bila yeye [kushinikiza], ilibidi tubadilishe kidogo majukumu tofauti ambayo tulikuwa tumezoea. Tulikuwa miongoni mwa timu zenye presha kubwa kabla ya [Ronaldo kujiunga],” alisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved