FIFPro, PFA zatishia mgomo wa wachezaji watakaoshiriki Kombe la Dunia la Klabu 2025

"Ratiba nyingi za soka zinahatarisha afya za wachezaji na kupunguza ubora wa mchezo huo..." Mkurugenzi mtendaji wa PFA amesema akiitaka FIFA kubadilisha kalenda ya Kombe la dunia la Klabu 2025

Muhtasari

•FIFPRO, pamoja na PFA na Shirikisho la Ligi za Dunia (WLA), wanaendelea kutishia hatua za kisheria ikiwa FIFA haitabadilisha kalenda baada ya kuidhinisha kombe la dunia la klabu.

•Wachezaji wa klabu zitakazoshriki mashindano hayo wameonya kuwa watashiriki mgomo ikiwa FIFA haitawaskiza.

 

Wachezaji wamelionya shirikisho la soka duniani FIFA kuwa wako tayari kugoma kutokana na mrundiko wa kalenda ya  mechi, hii ni baada ya kuidhinisha mashindano ya kombe la dunia la vilabu 2025.

Afisa mkuu Mtendaji wa muungano wa wanasoka wa kulipwa (PFA)  Maheta Molango alisema Alhamisi.  Muungano wa wachezaji duniani FIFPRO  kwa ushirikiano na ligi mbali mbali za ulaya waliwasilisha malalamishi yao kwa FIFA. 

Siku mbili kabla ya fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund jijini London, ligi kuu ya Uingereza, LaLiga, Serie A na PFA zilikutana ili kuchunguza hatua za kukabiliana na nia ya FIFA ya kuongeza idadi ya mechi ambazo wanasoka watalazimika kuvumilia msimu ujao ya kombe jipya la dunia la vilabu linalokaribia.

Mkurugenzi mtendaji wa PFA, Maheta Molango, ambaye amekuwa akitaka mabadiliko tangu Februari, anaamini kuwa wachezaji wamefikia pabaya. Anasema ratiba nyingi za soka zinahatarisha afya za wachezaji na kupunguza ubora wa mchezo wa soka.

"Mahitaji ya wachezaji yameongezeka katika miaka ya hivi majuzi, huku mashindano yakipanuka na mashindano mapya kuibuka, huku wachezaji na wasimamizi wakisema kwamba kalenda hiyo inataka mechi nyingi. " Molango alisema.

Muungano wa wachezaji wa kimataifa FIFPRO, pamoja na PFA na Shirikisho la ligi za dunia (WLA), wanaendelea kutishia hatua za kisheria ikiwa FIFA haitabadilisha mkondo. Katika barua iliyotumwa kwa rais wa FIFA Gianni Infantino na katibu mkuu Mattias Grafstrom, walielezea wasiwasi wao juu ya upanuzi wa michuano mipya ya kombe la dunia la vilabu yenye timu 32.

Aidha,FIFA ilikanusha madai yao kuwa imechukua maamuzi ya upande mmoja kupendelea mashindano yake katika kalenda ya kimataifa na haitafikiria kupanga tena mashindano.

Utafiti uliolenga wachezaji wachanga ulionya jinsi miili yao ilivyo na mkazo mwingi na kuangazia idadi ya dakika ambazo wamecheza. kwa mfano,kiungo wa  Real Madrid na Muingereza Jude Bellingham amecheza mechi mingi kabla ya kufikisha miaka 21. Kiungo huyo, bado ana umri wa miaka 20, amecheza dakika 18,486 katika maisha yake ya soka, ikilinganishwa na David Beckham 3,929 alizocheza na dakika 6,987  ambazo Frank Lampard alicheza katika umri huo huo.