Ten Hag kusalia Manchester United baada ya kushinda FA

Ten Hag aliwapiku kocha wengine kwa kuchaguliwa bora zaidi

Muhtasari

•Ten Hag atasalia Old Trafford na kwamba anatazamiwa kuongezewa mkataba, licha ya hofu ya hivi majuzi kwamba atapigwa kalamu

•Ushindi wa Ten Hag wa Kombe la FA na masuala ya majeraha ya kikosi ndio sababu kuu katika uamuzi wa yeye kusalia kama meneja

Kocha wa Man Utd Eric Ten Hag
Image: Hisani

Uhakiki wa mwisho katika klabu ya Manchester United umekamilika na imebainika bayana kuwa Erik ten Hag atasalia kama meneja wa klabu hiyo msimu ujao.

Habari hii ilizuka mnamo Jumanne usiku kwamba Ten Hag atasalia Old Trafford na kwamba anatazamiwa kuongezewa mkataba, licha ya hofu ya hivi majuzi kwamba atapigwa kalamu kufuatia msimu uliokamilika kwa msukosuko  na patashika 2023/24.

Mkataba wa sasa wa Ten Hag utakamilika mwishoni mwa msimu ujao huku klabu ya Manchester United ikiwa na chaguo la kuanzisha nyongeza nyingine ya miezi 12.

Inafahamika kuwa ushindi wa Ten Hag wa Kombe la FA na masuala ya majeraha ya kikosi ndio sababu kuu katika uamuzi wa yeye kusalia kama meneja wa kikosi hicho.

Ineos vilevile ilifurahishwa na jinsi meneja huyo alivyoendesha klabu hiyo licha ya kipindi kigumu msimu uliopita.

United na Ten Hag wanasemekana kuungana baada ya mapitio ya msimu wa klabu, mchakato ambao ulidumu kwa zaidi ya wiki mbili na kuwashuhudia makocha wengine kama vile Mauricio Pochettino kubanduliwa nje kwa jukumu hilo azizi.

Hakuna hata mmoja wa wagombea hao walionekana wanafaa zaidi kwa jukumu hilo kuliko huyo, Ten Hag.

Ineos itakuwa ikifanya mabadiliko kwenye mkataba wa United na Ten Hag.

Fauka ya hayo, meneja huyo mwenye asili ya uholanzi, amekosolewa kwa idadi ya wachezaji wake waliosajiliwa tangu kuwa meneja, huku Antony akionekana kama mmoja wa wachezaji wa bei ghali zaidi wa klabu hiyo.

TenHag pia aliwasajili Lisandro Martinez na Rasmus Hojlund.

Baada ya kumaliza katika nafasi ya nane katika Ligi kuu ya Uingereza msimu uliopita, anatarajiwa kwa hamu  na ghamu kufanya vyema zaidi msimu ujao - ila anapaswa kuwa bora zaidi.