Droo ya kufuzu Afcon 2025 kufanyika Julai 4 kule Afrika Kusini

Timu 48 zitakazochuana zitagawanywa katika makundi 12 ya wanne, huku mbili za kwanza katika kila kundi zikifuzu kwa Afcon 2025 nchini Morocco.

Muhtasari

•Droo ya kufuzu  mashindano ya Afcon 2025 inatazamiwa kufanyika Julai 4, jijini Johannesburg Afrika Kusini.

•Jumla ya timu 24 zinatazamiwa kufuzu kwenye mashindano hayo yanayoratibiwa kufanyika nchini Morocco.

Image: Hisani

Droo ya kufuzu mashindano ya Afcon 2025 itafanyika Julai 4,jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Jumla ya timu 48 ikiwemo Chad,Eswatini,Liberia na Sudan Kusini zitapangwa katika makundi 12 ya timu nne  kila moja ili kushindania nafasi za kufuzu kwa mashindano ya Afcon 2025.

Mechi hizo za kufuzu zinatazamiwa kuanza Septemba,2024 ili kuamua timu 24 zitakazoshiriki kwenye mashindano ya 2025,nchini Morocco.Wenyeji Morocco tayari washajinyakulia nafasi kwa kuwa mashindano yatafanyika kwao.

 Makala ya mwisho ya mashindano haya yalifanyika mwaka 2023 nchini Ivory Coast,huku wenyeji hao wakinyakua taji hilo kwa mara ya tatu baada ya kuwafunga wenzao Nigeria kwenye fainali.

Hata hivyo,tarehe za fainali za Afcon 2025 bado hazijatangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Hapo awali CAF ilijitolea kuandaa michuano yake bora ya wanaume mwishoni mwa msimu wa vilabu vya Ulaya,katika kipindi cha Juni-Julai.Wakati huo mechi za  kombe la klabu la dunia 2025 zitakuwa zikichezwa.

Mapema mwezi huu katibu mkuu wa CAF,Veron Mosengo-Omba aliambia BBC Sport Africa kwamba kupanga ratiba ni "ndoto" na akakiri kwamba huenda fainali za 2025 zikachezwa mapema 2026.

"Tunahitaji kuhakikisha kuwa tarehe ambazo tutakuwa tunachagua zitakuwa kwa maslahi ya wachezaji," Veron alisema.