Kocha wa Kenya Police Bullets Beldine Odemba , amesema kuwa watarejea kambini mapema ili kujitayarisha kwa michuano ya ubingwa wa wanawake wa Cecafa ambayo inatarajiwa kuanza mwezi Agosti nchini Ethiopia.
Akizungumza na Citizen TV, Odemba alisema kuwa wachezaji hao watalazimika kutenga muda uliosalia ili kuwa tayari kwa mashindano hayo.
Bullets walitawazwa mabingwa wa ligi ya wanawake ya FKF mnamo Jumatano, Juni 26,2020 ambapo walikamilisha ligi kwa kuwacharaza Bunyore Starlets 3-0.
“Tunafaa kuanza matayarisho mapema ipasavyo ili tuwe tayari kwa mashindano ambayo yatakuwa azizi na itachukua ushirikiano wa kila mmoja. Najua hawatakua na muda wa kutosha wa kupumzika ila hatuna budi,” alisema Odemba.
Kocha huyo, vilevile, alisema kuwa wanapanga kuimairisha kikosi chao ili wapate nguvu zaidi wanapolenga ubingwa wa kina dada wa CAF.
“Tunajua tuna kikosi kizuri ila tuna mashindano mengi ya kushiriki. Tayari, tumewapata wachezaji ambao watahitaji kuongeza nguvu zaidi kwenye timu katika idara mbalimbali,” alisema.
Police Bullets walishinda kombe lao la kwanza la ligi msimu huu baada ya kunyakua taji kutoka kwa washindi wa mwaka jana, Thika Queens.
Odemba alisema kuwa ushindi huo wa ligi ulikuwa umetokana na bidii na ushirikiano wa kila mja kwenye timu.
“Bidii na ushirikiano wa timu ndio ulitupa ushindi wa kombe la ligi. Kila mja aliwajibika katika mafanikio haya na tunatumaini zaidi siku za usoni,” alimalizia kocha huyo ambaye pia ni mkuu wa timu ya taifa ya Rising Starlets U20.