Arsenal wazindua jezi mpya za ugenini zenye asili ya kiafrika kwa msimu wa 2024/25

Nyota wa Nigeria, Nwankwo Kanu, ambaye aliichezea Arsenal mara 197 kati ya 1999 na 2004 alipendezwa na kuzinduliwa kwa jezi hio.

Muhtasari

•Arsenal wamezindua hii leo jezi yao ya ugenini inayoashiria uhusiano kati ya Arsenal na wafuasi wao wa kiafrika.

•Foday Dumbuya, mwanzilishi wa Labrum London alielezea furaha yake baada ya kuzinduliwa kwa jezi hio.

Jezi ya ugenini ya arsenal
Image: Arsenal

Arsenal wamezindua jezi yao mpya kabisa ya ugenini kwa msimu wa 2024/25, ikichochewa na mashabiki wa klabu hiyo kutoka Afrika.

Kwa kushirikiana na kundi la waingereza la Labrum London, seti hii ina msingi mweusi ambao umeakibishwa na mitindo ya Kiafrika yenye herufi nzito ambayo imeanzia kwapani na kutiririka chini hadi kwenye kaptura.

Mchanganyiko wa rangi nyekundu na kijani kibichi  kwenye  bega pamoja na  nembo ya adidas  inaashiria uhusiano kati ya Arsenal na wafuasi wao wa Kiafrika.

Foday Dumbuya, mwanzilishi wa Labrum London, alisema:

"Kama mhamiaji wa kizazi cha pili nilipokua London, nilitazama wachezaji wa ajabu wa Arsenal wenye urithi wa kiafrika. Wachezaji hawa walikuwa mifano ya ajabu kwangu, wakicheza mchezo kwa njia nzuri, lakini pia kuwakilisha jamii pana ambayo ninaungana nayo."

"Arsenal kama klabu ina uhusiano mkubwa na jamii hii, kwa hivyo ni wakati wa kujivunia sana kwangu kushirikiana nao katika muundo huu."

Nyota wa zamani wa Nigeria, Nwankwo Kanu, ambaye aliichezea Arsenal mara 197 kati ya 1999 na 2004, aliongeza:

"Ninajivunia kuwakilisha klabu yangu na urithi wangu kupitia muundo huu kutoka Labrum London. Ni shati nzuri sana. Ninapenda jinsi mifumo na mitindo. rangi zinawakilisha uhusiano wetu na wachezaji wenye asili ya kiafrika na wafuasi wetu katika jumuiya zetu za Islington na duniani kote.

"Inafurahisha kuona tunasherehekea uhusiano huu wa kipekee na muundo maridadi. Ninafurahi kuona timu zetu zikiivaa ugenini msimu ujao."