Kocha mkuu wa Manchester United ,Erik Ten Hag, amesema klabu hiyo inaendelea kutathmini hali ya beki mpya Leny Yoro na mshambuliaji Rasmus Hojlund.
Usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, wachezaji hao wawili walitolewa uwanjani katika dakika za mapema wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Arsenal iliyochezwa kwenye uwanja wa SoFi, jimbo la California, nchini Marekani.
Huku akizungumzia wasiwasi kuhusu majeraha ya wachezaji hao vijana, kocha Ten Hag alisema watasubiri kwa angalau saa 24 ili kujua hali ya wawili hao. Aliwataka mashabiki wa Man United kuwa na matumaini wakati wakisubiri kuona jinsi majeraha yalivyo.
"Tunapaswa kusubiri kwa zaidi ya saa 24 na kisha tutajua zaidi," Ten Hag aliwaambia waandishi wa habari Jumapili asubuhi.
Aliongeza, “Tulikuwa makini hasa na Leny, alifanya 50% tu kutoka kwenye vipindi vya mazoezi. Hebu tuwe na imani na tuone matokeo yake ni nini.”
Manchester United walimenyana na Arsenal katika mechi ya kirafiki iliyochezwa usiku wa kuamkia Jumapili ambapo walishindwa kwa mabao 2-1.
Hojlund alifunga bao pekee la Manchester United katika dakika ya 10 kabla ya kutolewa nje ya uwanja dakika sita baadaye baada ya kuumia.
Mchezaji mpya Leny Yoro pia hakumaliza kipindi cha kwanza cha mechi kwani alitolewa nje akiwa na jeraha katika dakika ya 35.