Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti amethibitisha kuwa timu yake haitafanya usajili tena msimu huu wa joto, kufuatia kuwasili kwa Kylian Mbappé na Endrick.
Madrid hata hivyo, walikosa kumsajili beki wa kati wa Ufaransa Leny Yoro, ambaye alichagua kujiunga na Manchester United badala yake.
Huku kukiwa na ripoti kwamba wababe hao wa Uhispania bado wako sokoni kutafuta beki wa kati kufuatia kuondoka kwa Nacho na Rafa Marín, Ancelotti alisema:
"Kikosi kimefungwa. Vallejo amerejea, Alaba anaendelea kupata nafuu...tuna mabeki wa kati vijana kama Joan, Jacobo na Raul [Asencio] ambao wanafanya mazoezi na wana ubora mwingi. Ninaamini tumefunikwa vyema katika nafasi hii."
Mkongwe Nacho hivi majuzi alisajiliwa na Al Qadsiah ya Saudi Arabia baada ya kumaliza ushirikiano wa miongo miwili na Madrid huku Marin, aliyecheza msimu uliopita kwa mkopo Deportivo Alavés, alijiunga na Napoli kwa uhamisho wa kudumu.
Madrid pia ilimpoteza mshambuliaji wa Uhispania Joselu, ambaye alihamia Al Gharafa ya Qatar.
Ancelotti, ambaye timu yake ilishinda LaLiga, ligi ya mabingwa na kombe la Super Cup la Uhispania msimu uliopita, hatarajii wachezaji wengine kuondoka.
"Hakuna atakayeondoka kwa sababu kila mtu anataka kubaki," Ancelotti alisema.Vile vile wakati huo huo, alikiri Madrid italazimika kuzoea kucheza bila Toni Kroos.
Kiungo huyo wa kati wa Ujerumani alistaafu soka baada ya Euro 2024 na kufurahia kukaa kwa miaka tisa Madrid.
"Tunamkosa Kroos," Ancelotti alisema. "Lakini tuna uwezekano wa kuchukua nafasi yake, ingawa kwa njia tofauti kwa sababu hakuna mchezaji kama yeye, na ubora wake.
"Lakini tuna rasilimali nyingine nyingi."
Madrid wanaanza ziara yao ya mechi za kirafiki nchini Marekani dhidi ya klabu ya zamani ya Ancelotti AC Milan hii leo Jumatano Julai 31,kwenye uwanja wa Soldier mjini Chicago,kisha wacheze na Barcelona kabla ya kucheza dhidi ya Chelsea mnamo Agosti 6.