Chelsea wamekamilisha usajili wa mlinda lango Filip Jorgensen kutoka klabu ya Villarreal inayoshiriki ligi kuu ya Uhispania.
Klabu hiyo yenye maskani London,ilithibitisha kuwa golikipa huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye msimu uliopita alikua kipa nambari moja wa Villarreal, amesaini mkataba wa sita.
Klabu haikufichua ada ya uhamisho lakini vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kuwa dili hilo lilikuwa na thamani ya karibu pauni milioni 20 ($25.67 milioni).
"Hatua hii ni ndoto iliyotimia," Jorgensen aliambia tovuti ya klabu.
"Nimefurahi sana kusaini Chelsea, moja ya klabu kubwa duniani. Siwezi kusubiri kujua kila mtu na kuanza kucheza na wachezaji wenzangu wote wapya."
Jorgensen alifanyiwa vipimo vya afya Marekani,ambako timu imepiga kambi kwenye matayarisho ya kujiandaa kabla ya msimu wa 2024/25 kung'oa nanga,na inaripotiwa pia tayari ameanza mazoezi.
Mzaliwa wa Uswidi kwa baba wa Denmark na mama wa Uswidi, Jorgensen aliwakilisha Uswidi katika viwango vya vijana kabla ya kuhamia Denmark mnamo Mei 2021.
Mechi yake ya kwanza katika ligi ya La Liga ilifuatiwa Januari 2023 na kabla ya kampeni za 2023/24, Jorgensen alijihakikishia nafasi kama kipa nambari moja wa Villarreal.
Alicheza mechi 37 katika mashindano yote msimu uliopita na kusaidia Villarreal kumaliza katika nafasi ya nane kwenye ligi kuu ya Uhispania.
Jorgensen anatarajiwa kuwania nafasi ya kwanza na Robert Sanchez huku mlinda lango Petrovic akitarajiwa kuondoka klabuni humo.
The Blues wamebakiza mechi tatu za kirafiki,kwa hivyo huenda,Jorgensen achezeshwe kwenye mechi dhidi ya Club America,Manchester City au Real Madrid kabla ya kusafiri London,kuanza shughuli pevu.
Chelsea wataanza kampeni yao ya Ligi Kuu wakiwa nyumbani dhidi ya mabingwa City Jumapili, 18 Agosti.