Mashabiki wa kabumbu haswa wanaoshabikia timu ya Manchester United kutoka Uganda, waliandaa hafla ya pamoja kwa ajili ya kumwombea kocha wa Man United Ruben Amorim. Hii ni kwa mujibu wa video iliyochapishwa katika mtandao wa Instagram kwenye ukurasa wa Watsuptv, inayohusika na habari za burudani.
Tangu kujiunga na Manchester United rasmi Novemnba 11, Ruben Amorim ameongoza timu kwa mechi moja pekee dhidi ya Ipswich Town Jumapili ya tarehe 24 Novemba, mechi ambayo ilikamilika kwa sare ya kufungana bao moja kwa moja.
Manchester United ipo katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali la EPL baada ya raundi 12 za msimu huu ikiwa imeshinda mechi nne, kupoteza nne na kutoka sare nne.
Mashabiki wa Manchester United wamezidi kuonyesha upendo kwa timu yao kwa kuandaa maombi hayo, miezi michache baada ya kujitokeza kwa wingi kumwona golikipa wa Manchester United Andrea Onana wakati wa mchuano wa kufuzu kombe la mataifa barani Afrika AFCON 2025, wakati wa mechi ya Cameroon katika uwanja wa Nelson Mandela dhidi ya Zimbabwe.
Ujio wa Ruben Amorim ulijiri baada ya kufutwa kazi kwa Eric Ten Hag kutokana na mwanzo mbaya wa ligi na timu ya Man United.
Hata hivyo, maombi hayo yanajiri baada ya Kocha Ruben Amorim kukiri kuwa Manchester United itakuwa na wakati mgumu kurejea katika hadhi yake ya kuweka matokeo mazuri kwenye mechi zake.
Baada
ya mechi dhidi ya Ipswich Town, Kocha Amorim alikiri kuwa timu hiyo itakuwa na wakati mgumu
kwenye ligi kwa muda mrefu kabla ya kuimarika na kuanza kuandikisha matokeo
bora.