logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kocha Nuno Santo Santo Akiri kutotumia Mabeki Wengi Kwa Sababu ya Arsenal Kukosa Mshambuliaji

Santo amefichua sababu ya kubadili mfumo wake wa ulinzi wakati wa mechi dhidi ya Arsenal Jumatano usiku.

image
na Samuel Mainajournalist

Football27 February 2025 - 07:38

Muhtasari


  •  Santo alisema hakuhitaji kuongeza beki wa ziada kwa sababu ya ukosefu wa mshambuliaji wa kawaida katika kikosi cha Mikel Arteta.
  • "Kwa sababu Arsenal haina mshambuliaji, na [Mikel] Merino akicheza katika nafasi hiyo - hakuna haja ya kuwa na mlinzi wa ziada," alisema.

Kocha Nuno Espirito Santo akizungumza na Martin Keown

Kocha wa Nottingham Forest, Nuno Espirito Santo, amefichua sababu ya kubadili mfumo wake wa ulinzi wakati wa mechi dhidi ya Arsenal mnamo Jumatano usiku.

Katika mahojiano baada ya mechi, Santo alisema hakuhitaji kuongeza beki wa ziada kwa sababu ya ukosefu wa mshambuliaji wa kawaida katika kikosi cha Mikel Arteta.

Forest na Arsenal walitoka sare tasa ya 0-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza iliyochezwa kwenye Uwanja wa City Ground Jumatano usiku.

Matokeo hayo yaliwawezesha Forest kusalia katika nafasi ya tatu, huku Manchester City ikipunguza tofauti ya alama hadi moja baada ya kushinda Tottenham 1-0.

Katika mahojiano na TNT Sports, Nuno alitoa kauli iliyoacha mshangao kwa mchezaji wa zamani wa Arsenal, Martin Keown.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake wa kutumia safu ya ulinzi ya mabeki wanne badala ya watano, Nuno alijibu kwa uwazi:

"Nitakuambia. Kwa sababu Arsenal haina mshambuliaji, na [Mikel] Merino akicheza katika nafasi hiyo - hakuna haja ya kuwa na mlinzi wa ziada. Idadi kubwa ya wachezaji ipo katikati ya uwanja, na lilikuwa ni suala la kudhibiti eneo hilo."

Licha ya Arsenal kuonesha kiwango cha juu cha kumiliki mpira, walishindwa kutengeneza nafasi za wazi, jambo lililoonesha madhara ya kutokuwa na mshambuliaji wa asili. Forest, kwa upande wao, walijipanga vyema na kufanikisha lengo lao la kutoruhusu bao, jambo lililomfurahisha Nuno.

Akizungumza na BBC Sport, Nuno alisifu mchezo wa kikosi chake akisema:

"Nina furaha kubwa kwa jinsi tulivyocheza dhidi ya Arsenal. Ni timu bora sana, na inahitaji juhudi kubwa kuwazuia. Tulikuwa imara na tulijipanga vyema. Baada ya kipindi kigumu cha kufungwa mabao mengi, ilikuwa muhimu kurudi kwenye misingi yetu - kuwa imara na kupata clean sheet."

Forest walikuwa na fursa chache za kushambulia lakini walionekana kuridhika na pointi moja dhidi ya Arsenal.

Upangaji wao wa ulinzi ulidhihirika kuwa wa mafanikio, huku wakiwazuia vijana wa Arteta kusababisha madhara makubwa.

Baada ya mechi hii, Nottingham Forest wataelekeza macho yao kwenye mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA dhidi ya Ipswich Town kabla ya kumenyana na Man City katika mchezo muhimu wa ligi.

Arsenal, kwa upande wao, watapata muda wa ziada wa kujiandaa kwa mchuano wao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSV Eindhoven, baada ya kutolewa kwenye FA Cup.

Je, Arsenal wataweza kupata suluhisho la ukosefu wa mshambuliaji wao au wataendelea kusumbuka? Muda utaamua.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved