
Baada ya miezi kadhaa ya kutafuta mtu wa kuchukua nafasi ya Edu Gaspar, hatimaye Arsenal wanaonekana kupata jibu sahihi.
Ripoti zinaeleza kuwa Andrea Berta, aliyewahi kuwa mkurugenzi wa michezo wa Atlético Madrid, yuko kwenye mazungumzo ya mwisho na Wanabunduki na huenda akatangazwa rasmi muda wowote wiki ijayo.
Andrea Berta, raia wa Italia mwenye umri wa miaka 52, ni mmoja wa wakurugenzi wa michezo wenye rekodi bora barani Ulaya.
Alijiunga na Atlético Madrid mwaka 2013 na baadaye kuwa mkurugenzi mkuu wa michezo mwaka 2017.
Chini ya usimamizi wake, Atletico walifanya usajili wa mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kumsajili Rodri kutoka Villarreal kwa pauni milioni 16.5 kabla ya kumuuza kwa Manchester City kwa takribani pauni milioni 62. Pia alihusika katika uhamisho wa nyota kama Antoine Griezmann, João Félix, na Luis Suárez, aliyesaidia Atlético kutwaa taji la La Liga msimu wa 2020/21.
Uwezo wake wa kusimamia biashara za usajili na kujenga vikosi imara ndio umemfanya kuwa chaguo la Arsenal, klabu inayotaka kushindana na timu kama Manchester City na Liverpool kwa mataji.
Berta ndiye anayependekezwa zaidi kuchukua nafasi ya Edu Gaspar ambaye aliondoka Arsenal mwaka jana baada ya kuhudumu kama mkurugenzi wa michezo kwa takriban miaka mitano.
Edu Gaspar alijiunga na Arsenal kama mkurugenzi wa michezo mwaka 2019 na alikuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha kikosi cha Mikel Arteta. Alihusika katika usajili wa wachezaji muhimu kama Gabriel Jesus, Oleksandr Zinchenko, Declan Rice, na Kai Havertz, ambao wameimarisha kikosi cha Arsenal katika mbio za ubingwa.
Hata hivyo, baada ya takribani miaka mitano Emirates, Edu alitangaza kuondoka mwezi Novemba 2024, akisema anatafuta changamoto mpya katika maisha yake ya kikazi.
Arsenal walianza mchakato wa kutafuta mrithi wake, na sasa Berta anaonekana kuwa mtu sahihi wa kuchukua nafasi yake na kusimamia masuala ya usajili na maendeleo ya kikosi.
Ikiwa Berta atakamilisha makubaliano na Arsenal, Wanabunduki watakuwa wamepata mmoja wa wakurugenzi wa michezo wenye uzoefu mkubwa barani Ulaya.
Mashabiki wa Arsenal watalazimika kusubiri tangazo rasmi, lakini matarajio ni makubwa kwamba atasaidia klabu hiyo kufanikisha usajili mzuri na kuendelea kuwa washindani wakubwa wa Ligi Kuu ya England na Ulaya kwa ujumla.