
Arsenal imepata habari njema baada ya nyota wake Bukayo Saka
kurejea mazoezini, ikiwa ni wiki moja kabla ya kuikabili Real Madrid kwenye
robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kurejea kwa Saka ni afueni kubwa kwa kikosi cha Mikel Arteta, ambacho kimekosa huduma yake kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na jeraha la msuli wa paja.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram siku ya Alhamisi, Saka alipakia picha akiwa mazoezini katika kambi ya London Colney, akiambatanisha na ujumbe mfupi lakini wenye maana kubwa: "Hello again". Hii ni ikisharia wazi kuwa kurejea kwake ni suala la muda mfupi tu.
Winga huyo wa mwenye umri wa miaka 22 alipata jeraha Desemba mwaka jana, hali iliyomlazimu kukaa nje kwa muda mrefu huku Arsenal ikiendelea na kampeni zake bila mmoja wa wachezaji wake muhimu.
Hata hivyo, kurejea kwake kunawapa Wanabunduki nguvu mpya hasa kuelekea mchuano mgumu dhidi ya mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa, Real Madrid.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka ndani ya Arsenal, Saka tayari ameshiriki mazoezi kamili na kikosi cha kwanza, na kuna uwezekano mkubwa wa kujumuishwa kwenye kikosi kitakachokabiliana na Fulham mnamo Aprili mosi katika Ligi Kuu ya Uingereza.
Hii itakuwa mechi ya majaribio kuona kama atakuwa fiti kwa asilimia mia moja kabla ya safari ya kuelekea Santiago Bernabéu.
Kurejea kwake ni afueni kubwa kwa Arteta, ambaye atahitaji
kikosi chake kuwa katika hali bora zaidi ili kupambana na Real Madrid.
Timu hiyo ya Carlo Ancelotti ina rekodi bora kwenye michuano hii, na Arsenal italazimika kuwa na wachezaji wake mahiri kama Saka ili kuwa na nafasi ya kufuzu kwa nusu fainali.
Ratiba ya Arsenal Inayomsubiri Saka
- Arsenal vs Fulham – Aprili 1, 2025
- Everton vs Arsenal – Aprili 5, 2025
- Real Madrid vs Arsenal (Ligi ya Mabingwa, Robo Fainali) – Aprili 8, 2025
- Arsenal vs Brentford – Aprili 12, 2025
- Arsenal vs Real Madrid (Marudiano) – Aprili 16, 2025
Mashabiki wa Arsenal wana matumaini kuwa Saka atakuwa tayari
kwa wakati ufaao, huku akitarajiwa kuwa moja ya silaha muhimu za Gunners katika
jitihada za kusaka mafanikio barani Ulaya.