
Kipa wa Manchester United, Andre Onana, amejipata katika vita vya maneno na kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Nemanja Matic, baada ya kutofautiana kuhusu ubora wa kikosi cha United kulinganisha na Lyon ya Ufaransa.
Mzozo huo ulianza baada ya Onana kueleza kuwa Man United ni “bora zaidi” kuliko Lyon, kabla ya timu hizo kukutana kwenye robo fainali ya Ligi ya Europa.
Kauli hiyo ilimkera Matic ambaye sasa ni kiungo wa Lyon, na hakusita kumshambulia vikali Onana wakati wa mkutano na wanahabari siku ya Jumatano.
“Namheshimu kila mtu, lakini ili
kusema maneno kama hayo, unahitaji kuwa na msingi wa kuyasema,” alisema Matic.
Aliongeza “Kama wewe ni mmoja wa makipa duni zaidi katika historia ya
Manchester United, unapaswa kuwa makini na kauli zako. Kama ingekuwa Van der
Sar, Schmeichel au De Gea wameyasema hayo, ningefikiria mara mbili. Lakini kwa
mtu kama huyo, haikubaliki.”
Onana hakukaa kimya. Kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), alijibu kwa maneno yaliyodai kuwa hakudhamiria kuidharau Lyon, huku akijivunia mafanikio yake binafsi akiwa na United.
“Kamwe singewahi kuidharau klabu
nyingine,” aliandika Onana.
“Tunajua mechi ya kesho itakuwa ngumu dhidi ya wapinzani imara. Lengo letu ni
kuandaa mchezo bora kwa ajili ya kuwapa mashabiki wetu furaha. Angalau mimi
nimebeba mataji na klabu bora zaidi duniani — si kila mtu anaweza kujivunia
hilo,” aliongeza
Onana alijiunga na Manchester United mwaka 2023 akitokea Inter Milan kwa dau la pauni milioni 47.2. Hadi sasa, amecheza mechi 93 na kuweka clean sheets 23, na pia ameshinda Kombe la FA.
Hata hivyo, msimu wake wa kwanza Old Trafford umekumbwa na lawama nyingi kutokana na makosa ya mara kwa mara golini, hali iliyomfanya akosolewe vikali na baadhi ya mashabiki.
Kwa upande wake, Nemanja Matic alichezea Manchester United kati ya mwaka 2017 hadi 2022 na kuonekana mara 128. Alikuwa na mafanikio makubwa akiwa Chelsea ambako alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu ya England, Kombe la FA na EFL Cup. Baada ya hapo, aliitumikia AS Roma na Rennes kabla ya kujiunga na Lyon mwaka huu.
Kwa sasa, Manchester United wapo
katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, na Ligi ya Europa
ndiyo nafasi yao ya mwisho kujiokoa msimu huu chini ya kocha Ruben Amorim.