
Kocha wa Newcastle United, Eddie Howe, hatakuwapo kwenye benchi la ufundi katika mechi mbili zijazo za Ligi Kuu ya Uingereza.
Hii ni baada ya Muingereza huyo mwenye umri wa 47 kuthibitishwa kuwa anaugua nimonia.
Howe alilazwa hospitalini siku ya Ijumaa baada ya kulalamikia hali ya kutokuwa vizuri kwa siku kadhaa.
Alilazimika kuitazama mechi ya Jumapili dhidi ya Manchester United akiwa kitandani hospitalini, ambapo kikosi chake kilipata ushindi wa kishindo wa mabao 4-1. Matokeo hayo yaliwapa Newcastle motisha mpya na kuwaweka tena kwenye mbio za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Licha ya kutokuwapo uwanjani, Howe aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo mkubwa ulioirejesha timu katika nafasi ya nne bora kwenye msimamo wa ligi.
Kupitia taarifa rasmi, Newcastle United imethibitisha kuwa kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa hatakuwepo katika mechi ya nyumbani dhidi ya Crystal Palace siku ya Jumatano, pamoja na mechi ya ugenini dhidi ya Aston Villa Jumamosi. Makocha wasaidizi Jason Tindall na Graeme Jones wataendesha mazoezi na kusimamia timu kwa sasa.
“Tunaweza kuthibitisha kuwa Eddie Howe anaendelea kupata nafuu hospitalini baada ya kugunduliwa kuwa na nimonia. Klabu inaendelea kutoa salamu za heri na kuunga mkono familia yake katika kipindi hiki,” ilisoma taarifa ya klabu.
Howe naye alitoa shukrani zake kwa mashabiki na wadau wa soka waliotuma salamu za pole na matumaini ya kupona haraka.
“Asanteni sana kwa ujumbe wa upendo na pole kutoka kwa mashabiki wa Newcastle United na jamii ya soka kwa ujumla. Ujumbe wenu umekuwa wa faraja kubwa kwangu na familia yangu,” alisema Howe.
Iwapo Newcastle itakwepa kipigo
dhidi ya Crystal Palace, basi itapanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa
ligi, mbele ya Nottingham Forest.