logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wanabunduki wawazima Mashetani Wekundu katika mechi ya kusisimua nchini Marekani

Mchezaji mpya wa United, Leny Yoro na mshambuliaji Rasmus Hojlund waliondolewa mapema baada ya kupata majeraha.

image
na SAMUEL MAINA

Michezo28 July 2024 - 06:11

Muhtasari


  • •Arsenal walilazimika kupambana kutoka nyuma baada ya mshambuliaji Rasmus Hojlund kuweka Man United mbele katika dakika ya 10.
  • •Mchezaji mpya wa United, Leny Yoro na mshambuliaji Rasmus Hojlund waliondolewa mapema baada ya kupata majeraha.
walipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Man United

Vilabu vikubwa vya Ligi Kuu ya Uingereza, Arsenal na Manchester United, vimemenyana katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa SoFi, Jimbo la California, nchini Marekani usiku wa kuamkia Jumapili.

Mechi hiyo ya kujiandaa na msimu mpya iliyosubiriwa kwa hamu ambayo  ilianza saa tisa asubuhi, masaa ya Afrika Mashariki ilishuhudia Wanabunduki wakiondoka na ushindi wa 2-1 dhidi ya mpinzani wao huyo wa muda mrefu.

Ushindi huo haukuwa rahisi kupatikanahata hivyo kwani vijana wa Mikel Arteta walilazimika kupambana kutoka nyuma baada ya mshambuliaji Rasmus Hojlund kuweka Man United mbele katika dakika ya 10.

Iliwachukua Arsenal dakika 26 kupata bao lao la kwanza kwenye mechi hiyo. Mshambulizi Gabriel Jesus aliifungia Arsenal bao la kwanza baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa chipukizi mahiri, Ethan Nwaneri.

Timu hizo mbili ziliendelea kuchuana vikali hadi Wanabunduki walipopata mafanikio katika dakika ya 81 kupitia kwa winga Gabriel Martinelli.

Mechi hiyo ilimalizika kwa Arsenal kushinda 2-1.

Hata hivyo, licha ya matokeo hayo, kulikuwa na mikwaju ya penalti ambayo Man United ilishinda kwa mabao 4-3.

Wakati wa mechi, vilabu vyote vilitoa nafasi kwa kikosi chao cha kwanza, wachezaji wa akiba na hata vijana kutoka akademi. Huenda hili lilifanywa ili kujaribu vikosi kabla ya msimu ya EPL 2024/25 unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Kwa bahati mbaya, mchezaji mpya wa Man United Leny Yoro na mshambuliaji Rasmus Hojlund waliondolewa katika dakika za mapema za mechi baada ya kupata majeraha.

Katika viwanja vingine, Man City ilifungwa mabao 2-3 na AC Milan katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Yankee, New York, Marekani. Aston Villa ilifungwa 1-4 na Columbus Crew ya Marekani na Wolves ikashinda 3-1 dhidi ya West Ham katika mechi zilizochezewa Marekani pia.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved