Mchezaji wa Kimataifa wa mchezo wa raga wa Kenya, Bernadette Olesia amefariki dunia.
Katika taarifa, Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilithibitisha kwamba mchezaji huyo alikata roho siku ya Jumanne asubuhi wakati alipokuwa anaendelea kupokea matibabu hospitalini.
Shirikisho hilo lilituma risala za rambirambi kwa familia ya marehemu, marafiki wake na wachezaji wenzake na kutangaza kuwa mipango ya mazishi itafichuliwa katika taarifa ya baadaye.
“Bernadette aliaga dunia Jumanne tarehe 15 Agosti 2023 alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini. Tunatuma rambirambi zetu kwa familia yake, marafiki, wafanyakazi wenzake na wenzake wa timu. Taarifa zaidi kuhusu mipango ya mazishi ya Bernadette itashirikiwa katika mawasiliano yajayo,” taarifa iliyotolewa na KRU Jumanne asubuhi ilisoma.
Shirikisho la Raga la Uganda pia lilimuomboleza marehemu Olesia na kumtambua kwa umahiri aliouonyesha wakati wa mechi ya Kenya vs Zambia katika michezo ya raga ya wanawake ya Afrika iliyofanyika Uganda mwaka jana.
“Tumehuzunishwa sana na taarifa za kuaga kwa mchezaji wa @OfficialKRU Bernadette Olesia ambaye pia alikuwa MVP (Kenya Vs Zambia) katika michezo ya raga ya wanawake ya Afrika tuliyoandaa mwaka jana. Tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia yake na wachezaji wenzake katika kipindi hiki kigumu,” URU ilisema.
Marehemu Bernadette alifanya kazi katika Shamas Rugby Foundation na alicheza raga ya klabu katika Shamas Rugby Foundation na timu ya wanawake ya Northern Suburbs.
Marehemu pia alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Kenya ya raga. Roho yake ipumzike kwa amani.