Chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka kimepata pigo lingine kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa David Musila.
Musila alikaribishwa Ijumaa kwenye chama cha Jubilee na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama hicho Kanini Kega.
Chama hicho kilisema kuwa Musila atawania kiti cha ugavana wa Kitui katika uchaguzi wa Agosti 9.
Haya yanajiri siku chache baada ya kamati ya kampeni ya Musila kukanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba anakaribia kugura kwenye Wiper.
"Habari iliyochapishwa na Star mnamo Jumatatu kuhusu Musila kujiondoa chama cha Wiper sio kweli na ni nukuu potofu," mwenyekiti Paul Kitungu alisema Jumatatu.
Alisema wafuasi wa Musila ndio waliochukua kipaza sauti na mmoja baada ya mwingine kumtaka mgombea huyo kuwania uchaguzi kama mgombea huru endapo mambo yatakuwa magumu Wiper.
Musila alizindua manifesto yake siku ya Jumamosi katika bustani ya Musila mjini Mwingi.
Yeye ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa chama cha Wiper pamoja na Kalonzo, aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama na Mutula Kilonzo Junior.