ODM yaahirisha uchaguzi wa mchujo Nakuru

Muhtasari

• Kupitia taarifa kwa wawaniaji wote Alhamisi usiku, Mumma alisema chama kilikuwa kimefutilia mbali kura za mchujo zilizopangwa kufanyika leo Aprili 1. 

Catherine Mumma mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya ODM
Catherine Mumma mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya ODM
Image: HISANI

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya ODM Catherine Mumma ameahirisha mchujo wa chama hicho mjini Nakuru kwa sababu alizosema ni za kiusalama. 

Kupitia taarifa kwa wawaniaji wote Alhamisi usiku, Mumma alisema chama kilikuwa kimefutilia mbali kura za mchujo zilizopangwa kufanyika leo Aprili 1. 

Bodi ya ychaguzi ilibaini kwamba hatua hiyo ilinuia kulinda maisha ya wanachama na viongozi na kwa hivyo iliwalazimu kusitisha kura za mchujo. 

Alitoa mfano ambapo maafisa Wasimamizi na makarani walipokea vitisho vya usalama kutoka kwa baadhi ya watu. Uamuzi wa uwakilishi wa wadi za Kaptembwa, Olkaria, Kivumbini na Shabaab utatolewa baadaye na kuwasilishwa kwa Wagombeaji. 

“Habari za jioni timu ya Nakuru!Hii ni kukufahamisha kuwa imetubidi kuahirisha uteuzi wa mchujo wa chama eneo la Nakuru na kuwasilisha uamuzi huu kwa kamati kuu,” taarifa bodi ya chaguzi ilisema. 

Mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi aliomba radhi wawaniaji wote walioathiriwa na hatua hiyo lakini akasisitiza kwamba maisha yalikuwa muhimu sana.  

Hapo awali, wawaniaji na maafisa wa ODM katika kaunti walikuwa na kikao cha faragha na kuibua wasiwasi kuhusu waliochaguliwa kusimamia kura za mchujo.