Kidero kutangaza mwelekeo mpya baada ya Gladys Wanga kupewa tiketi ya ODM

KIDERO-1
KIDERO-1

Aliyekua gavana wa Nairobi Evans Kidero ambaye ana azma ya kuania ugavana wa Homa Bay amesema kwamba atatangaza mwelekeo wake mpya baada ya ODM kumpokeza tiketi ya moja kwa moja Gladys Wanga kuania wadhifa huo.

Kidero katika ujumbe wake muda mfupi baada ya Wanga kupokezwa tiketi hiyo alisema  kwamba watu wa Homa Bay kwa mara nyingine tena wamenyimwa fursa ya kuchagua mgombeaji wa Chama cha ODM wanayempendelea kwa kiti cha ugavana kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9 2022.

 “Hili ni jambo la kusikitisha kwa sababu Homa Bay ililipia gharama wakati Dkt. Odhiambo Mbai, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Ugatuzi katika Kamati ya Kitaifa ya Marekebisho ya Katiba ya  Bomas, alipouawa na wale waliopinga mabadiliko ya Katiba. Tunastahili bora zaidi,” Kidero alisema. 

Kidero aliongeza kuwa, “Kama mwana na mpiga kura aliyesajiliwa katika Kaunti ya Homa Bay nitafuata njia mbadala ili kuwapa wapiga kura fursa nyingine ya kumchagua kiongozi wanayemtaka mnamo Agosti 9, 2022.” 

Gavana huyo wa kwanza wa kaunti ya Nairobi alikashifu kile alitaja kama watu saba waliokutana katika hoteli moja jijini Nairobi kuwaamulia wakazi zaidi ya milioni moja wa Kaunti ya Homa Bay.

 “Nia zao zinajulikana. Sikujulishwa wala kualikwa kwenye mkutano huu ambapo mamlaka na uhuru wa wapiga kura wa Homa Bay yalidhalilishwa,” Kidero alisema. 

Uchaguzi wa mchujo kumteua mgombeaji wa ugavana kwa tiketi ya ODM katika kaunti ya Homa Bay ulikuwa umeratibiwa kufanyika Aprili 14, 2022 na Kidero alisema kwamba wananchi wa kaunti hiyo wangepewa nafasi kuchagua mgombeaji wanayemtaka. 

Kidero alisema lengo lake kuania ugavana wa Homa Bay lilikuwa kuona Kaunti hiyo ikiimarika kutoka hadhi yake ya sasa hadi kufikia kiwango ambacho wakazi wanaweza kufurahia matunda ya ugatuzi. 

Amewaomba wakazi wa kaunti hiyo kudumisha amani na utangamano na kusubiri mweleko atakao uchukuwa. 

Chama cha ODM siku ya Alhamisi kiliwakutanisha wagombeaji saba waliokuwa wamewasilisha maombi ya kutaka kuwania ugavana kwa tiketi ya ODM chini ya uwenyekiti wa kinara wa chama hicho Raila Odinga na kuafikia kumpa tiketi mwakili wa wanawake Gladys Wanga naye Oyugi Magwanga akitajwa kama mgombea mwenza wake.