Gari la kampeni la Chris Wamalwa lagonga na kumuua mwanamke-Kiminini

Onditi alisema maafisa wa polisi walifika mapema kwenye tukio na kurejesha hali ya usalama.

Muhtasari

•Gari la kampeni linasemekana kumwangusha mwanamke ambaye hakutambulika na kumuua papo hapo - polisi walithibitisha.

•Dereva aliyejeruhiwa anaendelea kupata nafuu katika hospitali ya Kiminini Cottage.

Gari la kampeni la Chris Wamalwa ambalo lilihusika kwenye ajali.
Gari la kampeni la Chris Wamalwa ambalo lilihusika kwenye ajali.
Image: Facebook

Wenyeji waliokuwa na hasira kutoka  Kiminini katika Kaunti ya Trans Nzoia mnamo Jumatano usiku Juni 29 2022 waliteketeza lori la Mbunge wa Eneo bunge la Kiminini na mgombea mtarajiwa wa ugavana wa Trans Nzoia Chris Wamalwa.

Gari la kampeni linasemekana kumwangusha mwanamke ambaye hakutambulika na kumuua papo hapo - polisi walithibitisha.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kiminini, John Onditi alisema ajali hiyo mbaya ilitokea baada ya gari hilo kutumbukia kwenye mtaro.

"Kilichotokea ni ajali ya kawaida ya trafiki ambayo ni mbaya. Ilimuua mwanamke na wenyeji wenye hasira walimiminika eneo la tukio na kuteketeza gari. Mguu wa dereva pia ulivunjika katika ajali hiyo," Onditi alithibitisha.

Onditi alisema maafisa wa polisi walifika mapema kwenye tukio na kurejesha hali ya usalama.

"Tulikimbilia kwenye eneo la tukio na tulipofika, gari lilikuwa tayari limeteketezwa. Tangu wakati huo tumeweza kurejesha hali ya usalama  hapa," aliongeza.

Dereva aliyejeruhiwa anaendelea kupata nafuu katika hospitali ya Kiminini Cottage.

Chris Wamalwa kupitia kwa ukurasa wake wa Twitter alionyesha masikitiko yake na kurai wakazi kumwombea  familia iliyoachwa.

''Natoa pole kwa familia na marafiki wa marehemu Florence Apondi, aliyefariki kufuatia ajali mbaya ya barabarani, iliyohusisha gari langu moja la kampeni,'' kwenye chapisho.

Mwili wa mwathiriwa ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kitale ukisubiri kufanyiwa upasuaji.