Aliyekuwa seneta wa kwanza wakaunti ya Kakamega Boni Khalwale amejipata katika kashfa kali baada ya kupakia picha kwenye ukurasa wake wa Twitter akiwa amebebwa na baiskeli huku akidai kwamba mwendesha baiskeli ile alimwitisha shilingi 20 tu pesa za Kenya ili kumzungusha katikati mwa mji wa Kakamega.
“Maisha yanaendelea. Mwendesha baiskeli huyu kwa furaha anatoza 20/= kwa safari moja ndani ya Mji wa Kakamega,” Khalwale aliandika.
Watu wamemsuta vikali mwanasiasa huyo huku wakidai kwamba hafai kulipa shilingi ishirini kwa mwenye baiskeli hiyo kwani shilingi ishirini ni kama dharau kwa mtu kutokana na hali ngumu ya kiuchumi huku mfuko wa kilo mbili wa unga ugali ukiwa ni zaidi ya shilingi 200 pesa za Kenya.
“Unapaswa kuwa na wasiwasi sana bwana! Anatakiwa kufanya zaidi ya safari 15 ili kumudu kilo 2 za Unga. Hakuna hadhi hapo,” mmoja alimponda Khalwale kwa kauli yake.
Wengine walimtupia maneno kwamba huyo mfanyibiashara ako sawa ila sasa yeye na mrengo wake wanataka kumrudisha nyuma kutoka kwa baiskeli hadi kwa toroli, huku wakimaanisha kwamba chama ambacho Khalwale anawania nacho ni cha naibu rais William Ruto, UDA ambacho nembo yake ya utambulisho ni toroli.
“Kwa hiyo badala ya kumpandisha daraja na kuinua biashara yake kwa kumpa pikipiki unataka kumpa toroli!” aliandika mwingine.
Khalwale analenga kurudi katika kiti chake cha useneta kwa tikiti ya chama cha UDA baada ya kuachia kiti hicho kwa seneta wa sasa Cleophas Malala ambaye alipatqa mteremko katika uchaguzi wa 2017 pale ambapo Khalwale aliendea kuwania ugavana katika kaunti ya Kakamega.
Awali, Khalwale alikuwa na azma ya kuwania ugavana ila baada ya mashauriano ya kina, walikubaliana na Malala ili yeye arejelee useneta huku Malala akiendea ugavana kumrithi gavana wa sasa Wycliffe Oparanya.