logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Wachana na mimi! usidhuru watoto wangu!"- Ruto amfokea Uhuru

Ruto alisisitiza kuwa alimsaidia rais Kenyatta kupata uongozi na kumtaka kuonyesha shukran.

image
na Samuel Maina

Uchaguzi29 July 2022 - 12:25

Muhtasari


  • •Naibu rais William Ruto alimrai bosi wake kudumisha heshima kati yao na kumuomba asidhuru watoto wake.
  • •Ruto  alimwambia rais Uhuru kuwa hahitaji uungwaji mkono wake na kumtaka amwache peke yake.

Vita kati ya rais Kenyatta na naibu wake William Ruto vimeendelea kuchacha huku uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ukiwadia.

Ugomvi wa wakuu hao wa nchi wawili umechukua mkondo mpya huku Ruto sasa akimshtumu rais kwa kutishia maisha yake.

Akizungumza mjini Kapsabet Ijumaa, naibu rais alimrai bosi wake kudumisha heshima kati yao na kumuomba asidhuru watoto wake.

"Rafiki yangu bwana rais, tafadhali kuwa muungwana. Kuwa na shukrani, sisi ndio tulikusaidia.  Tafadhali.. Wacha kujifanya saa hizi sijui unajifanya nini. Eti sasa wewe unaanza kunitishia mimi! Eti utanifanya nini.. bora usidhuru watoto wangu. Lakini mimi na wewe tuheshimiane tafadhali," Ruto alisema.

Naibu rais pia alisisitiza kuwa alimsaidia rais kupata uongozi na kumtaka kuonyesha shukran kwa usaidizi wake.

"Hufai kuwa chanzo cha vitisho Kenya. Wacha kutisha Wakenya. Kazi yako ni kuhakikisha Wakenya wako salama. Wacha kutuambia ati tutakujua wewe ndiye rais. Sisi ndio tulikuchagu uwe rais wa Kenya. Wacha kututisha. Sisi sio watu wa kutishwa," Alisema.

Ruto vilevile alibainisha kuwa hana mpango wowote wa kulipiza kisasi kwa rais licha ya ugomvi uliojitokeza kati yao.

Alimwambia Uhuru kuwa hahitaji uungwaji mkono wake katika kinyang'anyiro kijacho na kumtaka amwache peke yake.

"Mimi ni Mkristo. Mimi sitakuwa na maneno na wewe. Nitahakikisha kuwa umeenda nyumbani polepole na upumzike uendelee na maisha yako uniachie Kenya hii niiskume mbele," Alisema.

"Wachana na William Ruto. Nilikuunga mkono wakati ulinihitaji. Kama hutaki kuniunga mkono niache! Tafadhali!"

Haya yanajiri siku moja baada ya rais kumshambulia naibu huyo wake akimshutumu kwa kile alichokitaja kuwa "kueneza uwongo wa wazi" kwa wananchi.

Akihutubia wakazi wa Nakuru siku ya Jumatanu , rais Uhuru alisema Ruto hawezi kuaminiwa na uongozi wa nchi.

Uhuru alisema naibu wake amekuwa akiuza uwongo na kuwataka wananchi kukaa wamoja na kutoyumbishwa na siasa ndogo ndogo.

Kuhusu BBI, rais alisema naibu wake aliwadanganya wananchi kwamba mpango huo haukuwa mzuri kwao hivyo basi kuwanyima rasilimali zaidi ambazo zingeweza kuleta usawa.

"Mtu fulani aliwaambia kuwa BBI ilikusudiwa kuniongezea muda wa kukaa, lakini nitarudi nyumbani siku chache zijazo. BBI ilikuwa muhimu kwa watu wetu kwa sababu ingeweza kuleta usawa. Watu wanapigana kwa sababu ya rasilimali," alisema.

Rais pia alimsuta Ruto kwa kuwadanganya wakazi wa Mombasa na Naivasha kuhusu reli ya kiwango cha standard gauge na bohari ya kontena ya Inland.

"Nataka tuambiane ukweli sababu ukweli utakuweka huru. Tumekuwa na rafiki yangu na mimi sichukii mtu yoyote hata kidogo, lakini sipendi mtu wa uongo."

Rais pia alitoa wito wa kuwepo kwa umoja na amani hapa nchini wakati uchaguzi mkuu unapokaribia.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved