Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati amewaambia wagombeaji wasio urais ambao wanajua wameshindwa katika uchaguzi wa Agosti 9 kukubali.
Akijibu swali la vyombo vya habari juu ya uhakika wa matokeo wanayotumia, mwenyekiti huyo aliwasihi baadhi ya wagombea kukubali kushindwa, mwenyekiti huyo alisema matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa katika ngazi ya jimbo ni ya mwisho.
'Nataka kuamini kwamba wanaokubali ushindi, ni kwasababu tayari wameshapokea matokeo yao. Ukijua matokeo yako na imedhibitiwa na maajenti wako na wamekupa fomu za matokeo unasubiri nini?" Chebukati alisema.
Wagombea kadhaa wamekubali kushindwa kulingana na matokeo yaliyotolewa katika vituo vya kujumlisha kura za maeneo bunge.
Miongoni mwao ni pamoja na Naomi Shaban (kiti cha Mbunge wa Taveta), Moses Kuria (kiti cha ugavana Kiambu) na Joshua Kutuny (kiti cha mbunge wa Chereng'any).
Wengine ni Mbunge wa Nyaribari Chache Richard Tong’i na Mbunge wa Embakasi Magharibi George Theuri.
Chebukati pia alisema matokeo yaliyojumlishwa yanaweza kupatikana kwa mtu yeyote kwenye tovuti ya matokeo ya umma.
"Mitandao ya kijamii, vyombo vya habari vya kawaida, waangalizi na watu wengine wanaovutiwa na mchakato huu wanapata maelezo kutoka kwa tovuti ya umma. Tovuti ya umma ina Fomu 34As, ambazo ni fomu zile zile ambazo pia zinashirikiwa na tume nyuma yetu," alisema
Mkutano huo wa Jumatano huko Bomas ulikuwa wa pili tangu upigaji kura kufungwa Jumanne saa kumi na moja jioni.