Mwanasheria Nelson Havi amekuwa wa hivi punde kujiunga kwenye orodha ndefu ya wanasiasa wanaotangaza kukubali kushindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Havi alitangaza kwamba ameshindwa katika uchaguzi wa eneo bunge Westlands na mbunge wa sasa Timothy Wanyonyi ambaye alikuwa anatetea kiti hicho kwa tikiti ya chama cha ODM.
“Hongera sana Team Havi. Sisi ni wachache katika mashindano ya Westlands. Wengi walimchagua Timothy Wanyonyi. Wanamstahiki ipasavyo katika hekima zao au ukosefu wake. Kwa upande wetu, tumeridhika na matokeo. Hongera sana wewe kaka yangu mkubwa, Tim Wanyonyi. Tumikia wananchi vizuri,” Havi aliandika kwenye Twitter yake Jumatano alasiri.
Havi aliachia ngazi yake kama mkuu wa chama cha wanasheria na kuwania ubunge Westlands kupitia chama cha UDA ambapo alitarajia kuwa mbunge mpya baada ya awali Wanyonyi kutangaza kwamab azma yake ilikuwa kuwania ugavana Nairobi.
Aidha baada ya mashauriano ya muda miongoni mwa vyama tanzu ndani ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, waliafikia kwamba Wanyonyi arudi katika nafasi yake kutetea kiti chake cha ubunge Westlands huku nyadhifa ya ugavana ikienda kwa Polycarp Igathe kutoka Jubilee ambaye anawakilisha muungano huo katika kinyang’anyiro cha ugavana kumenyana na Johnson Sakaja wa UDA.
Havi sasa ameingia kwenye orodha ya wanasiasa kama George Theuri aliyetangaza kukubali kushindwa Embakasi West, Nixon Korir aliyetangaza kukubali matokeo Lang’ata miongoni mwa wanasiasa wengine wengi.