Machafuko na hali ya sintofahamu vilishuhudiwa katika eneo bunge la Matuga baada ya wagombea watatu wa ugavana wa Kwale kuvamia chumba cha kuhesabu kura.
Watatu hao; Hamadi Boga (ODM), Chirau Ali Mwakwere (Wiper) na Lung'anzi Chai Mangale (PAA) walitaka shughuli za kujumlisha kura zisitishwe.
Wakiongozwa na Mwakwere, wagombea hao walidai kuwa zoezi zima la uchaguzi lilikumbwa na kasoro za uchaguzi.
Alisema wana ushahidi mkubwa wa njama za siri za kuchakachua kura hizo.
“Tuna taarifa halali za masanduku ya kura kusafirishwa hadi kwenye vituo vya kujumlisha kura bila mihuri,” alisema.
Mwakwere alisema zoezi hilo halikufanyika kwa uhuru na haki hivyo ni lazima kujumlisha kura kusitishwe hadi malalamiko yao yatakapotatuliwa.