Mgombea urais kwa tikiti ya chama cha Agano David Mwaure amekuwa mgombea urais wa kwanza kati ya wanne walioidhinishwa na IEBC Kukubali matokeo katika kile amekitaja kuwa ni baada ya kuona matokeo hayaegemei upande wao, wameamua kukubali kwamba hiki kiti si chao.
Akizungumza na wanahabari Jumapili adhuhuri, Mwaure alisema kwamba baada ya kuona matokeo hayo jinsi yanavyozidi kutolewa na IEBC na kujadiliana kwa undani na wanachama, wameamua kukubali mapema hata kabla ya mchakato mzima wa kuhesabu kura haujakamilika rasmi katika ukumbi wa Bomas.
“Tunachukua hatua hii baada ya kuona jinsi tulivyofanya katika uchaguzi na pia baada ya kujadili na timu yetu pale Bomas. Pia tumekuwa tukifuatilia jinsi mchakato wa kuhesabu wa kudhibitisha kura umekuwa ukiendelea kwenye ukumbi wa Bomas na kwamba takwimu zile zimekuwa zikimuegemea William Ruto, ambaye ni naibu wa sasa wa Kenya. Sasa hivi tukikubali matokeo, kitu ambacho tumefanya, tungependa kuwashukuru familia zetu, na timu ya kampeni zetu kwa kusimama na sisi,” Mwaure alisema.
Mhubiri huyo vile vile alizidi mbele kuisihi tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kusimama imara na kutopindishwa na vikwazo au vitisho vyovyote kutoka kwa mrengo wowote kwani Wakenya wanatarajia matokeo ya ukweli na haki.
“Tukiwa tumejitoa katika mbio hizo, tungependa kumpendekeza yule anayeonekana kuwa kifua mbele, Dkt William Samoei Ruto na kuitaka IEBC kusimama imara kumtangaza kuwa mshindi wakati wake ukifika, mimi na mgombea mwenza wangu sasa tumetangaza kwamba tutaungana naye William Ruto na kumuunga mkono sio tu kwa sababu anashinda ila pia manifesto yake inawiana na yenu,” Mwaure alisema.