IEBC inapokaribia kutangaza washindi wa viti vya useneta baadhi ya viongozi walifanikiwa kuhifadhi viti vyao.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, maseneta wengi walihifadhi viti vyao.
Kaunti ya Mombasa
Mohamed Faki alishinda dhidi ya wapinzani wake kuhifadhi kiti chake.
Faki, ambaye aliwania kwa tikiti ya ODM, alipata kura 110,040 huku mshindani wake wa karibu Hamisi Mwaguya wa UDA akipata kura 76,069 katika kinyang'anyiro kilichovutia wagombeaji 14.
Hii ni mara yake ya pili kuchaguliwa kwa kiti hicho baada ya kushinda kwa mara ya kwanza mwaka 2017.
Kaunti ya Kwale
Issa Juma Boy wa ODM alichaguliwa tena kwa kuzoa kura 52, 772.
Alifuatiwa na Antony Yama wa UDA aliyepata kura 41, 762 na Mudzo Nzili (1,250).
Wengine ni Salim Mwadumbo wa ANC alipata kura 16, 902 na William Ndeti wa DP kura 9,236.
Takriban wagombea tisa walijitokeza kuwania kiti cha useneta.
Kaunti ya Kilifi
Stewart Madzayo alichaguliwa tena kuwa Seneta wa Kilifi kwa tiketi ya ODM.
Kaunti ya Taita Taveta
Mwaruma Johnes Mwashushe ni Seneta wa Taita Taveta kwa muhula wa pili.
Mwalimu huyo wa zamani aliingia Seneti mnamo 2017.
Kaunti ya Garissa
Abdulkadir Haji alitangazwa kuwa Seneta mteule wa Garissa baada ya kupata kura 72,383.
Haji aliwania kiti hicho chini ya Jubilee na takriban wagombea wanane waliwania kiti cha useneta.
Kaunti ya Isiolo
Seneta Dullo Fatuma Adan alitetea kiti chake cha useneta katika uchaguzi wa Agosti 9.
Aligombea kwa tiketi ya Jubilee.
Alikuwa naibu kiongozi wa wengi katika Seneti ya pili na mwanamke wa kwanza kuwa Seneta wa Isiolo.
Kaunti ya Kitui
Seneta Enoch Wambua alitetea vyema kwa tiketi ya Wiper.
Kaunti ya Samburu
Seneta Steve Lelegwe ametetea kiti chake baada ya kujizolea kura 40,066 kwa tiketi ya UDA.
Alimshinda Joseph Lepariyo wa ODM aliyepata kura 2,111 huku Joshua Leparachao wa DAP-K akipata kura 485.
Kaunti ya Elegeyo Marakwet
Kipchumba Murkomen alitetea kiti chake cha useneta katika Elgeyo Marakwet kwa kupata kura 141,091.
Mpinzani wa Murkomen, gavana anayeondoka Alex Tolgos ambaye alikuwa anawania kwa tikiti ya Jubilee alifanikiwa kura 20,648.
Kaunti ya Nandi
Seneta wa Nandi Samson Cherargei alitetea kiti chake kwa tiketi ya UDA na kuibuka mshindi.
Kaunti ya Narok
Seneta wa sasa wa Narok Ledama Olekina amechaguliwa tena kuhudumu kwa muhula mwingine wa miaka mitano.
Ledama alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 135,180.
Alikuwa akigombea ODM. Gavana anayeondoka Samuel Tunai aliibuka wa pili kwa kura 117,869.
Tunai aligombea kwa tiketi ya UDA.
Ledama alikuwa miongoni mwa wawaniaji waliopewa tikiti moja kwa moja na ODM.
Kaunti ya Kericho
Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot ametetea kiti chake kwa tiketi ya UDA.
Kaunti ya Bungoma
Seneta wa Bungoma Moses Wetang'ula pia amechaguliwa tena.
Matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka yalionyesha kuwa bosi wa Ford Kenya alipata kura 286,143.
Kaunti ya Homa Bay
Seneta Moses Kajwang wa ODM alihifadhi kiti chake baada ya kupata kura 353,882.
Kajwang alimshinda Tom Ojanga wa Kanu aliyepata kura 18,290 huku Kenneth Kambona akiwa na kura 17,775.
Kaunti ya Machakos
Agnes Kavindu Muthama wa Wiper ametangazwa mshindi wa kiti cha useneta wa Machakos na IEBC.
Kavindu amekuwa seneta wa tatu wa Machakos baada ya kushinda uchaguzi mdogo wa 2021 kufuatia kifo cha Seneta Boniface Mutind Kabaka Disemba 2020.
Kaunti ya Nyamira
Seneta Okong’o Omogeni alihifadhi kiti chake baada ya kuzoa kura 96,432 dhidi ya Mose Nyambega wa UDA aliyepata kura 43,866.
Adams Mochenwa wa DP alikuwa wa tatu kwa kura 22,235.