Ubalozi wa Marekani waipongeza Kenya kwa uchaguzi wa amani

IEBC ilimtangaza Ruto mwenye umri wa miaka 55 kama rais mteule wa Kenya.

Muhtasari

• Ubalozi huo pia umewapongeza wananchi wa Kenya kwa kutumia haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi wa tarehe 9 Agosti.

Balozi wa Marekani nchini Kenya Margaret Whitman wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Ubalozi wa Marekani, Gigiri mnamo Agosti 7, 2022. Picha: ANDREW KASUKU
Balozi wa Marekani nchini Kenya Margaret Whitman wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Ubalozi wa Marekani, Gigiri mnamo Agosti 7, 2022. Picha: ANDREW KASUKU

Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umewapongeza Wakenya kwa mchakato wa amani, utaratibu wa upigaji kura na kuhesabu kura wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Ubalozi huo pia umewapongeza wananchi wa Kenya kwa kutumia haki yao ya kupiga kura katika uchaguzi wa tarehe 9 Agosti.

Katika taarifa yake, Marekani ilipongeza juhudi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, vikosi vya usalama, na taasisi za uchaguzi zilizoandaa mchakato mzima wa kura.

Iliwataka viongozi wote wa kisiasa kuwahimiza wafuasi wao kubaki watulivu na kujiepusha na ghasia.

"Chini ya uongozi wa Mwenyekiti Wafula Chebukati, IEBC ilimtangaza William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais," walisema.

“Hii ni hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi. Tunaomba pande zote zishirikiane kutatua kwa amani kero zozote zilizosalia kuhusu uchaguzi huu kupitia taratibu za sheria.”

Ubalozi huo pia ulipongeza ushiriki mkubwa wa vyama vya siasa vya Kenya, mashirika ya kiraia na wananchi kwa kujihusisha, kuunda, na kuwa na mijadala ya busara katika kipindi chote cha kampeni.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ilimtangaza Ruto mwenye umri wa miaka 55 kama rais mteule wa Kenya mnamo Agosti 15, 2022.

Ruto alihitaji asilimia 50 na kura moja juu, na asilimia 25 ya kura katika angalau kaunti 24 ili kutangazwa rais.

Alipata kura 7,176,141 ikiwa ni asilimia 50.49 ya kura, huku Raila Odinga wa Azimio aliyeshika nafasi ya pili alipata kura 6,942,930 ikiwa ni asilimia 48.85.