Chebukati ataka kukamatwa kwa waliohusika na machafuko ya Bomas

"Unyanyasaji huu lazima ukomeshwe mara moja," Chebukati alisema.

Muhtasari

• Aidha alisema baadhi ya wafanyikazi wa tume ya IEBC wametishwa na kunyanyaswa na kukamatwa kiholela.

akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akizungumza katika Bomas of Kenya mnamo Agosti 9, 2022
Image: ENOS TECHE

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati anataka kukamatwa mara moja kwa watu waliosababisha fujo katika ukumbi wa Bomas of Kenya siku ya Jumatatu.

Wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya urais, Chebukati na makamishna Abdi Guliye, Boya Molu na Mkurugenzi Mtendaji Hussein Marjan walishambuliwa na kujeruhiwa.

"Tunatoa wito wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka dhidi ya wavamizi hawa bila kujali mirengo yao ya kisiasa," Chebukati alisema Jumatano.

Aidha alisema baadhi ya wafanyikazi wa tume ya IEBC wametishwa na kunyanyaswa na kukamatwa kiholela.

"Hii imeweka hofu kwa wafanyakazi, ambao sasa hawawezi kuripoti ofisini kwa kazi," aliongeza.

Chebukati alitoa wito kwa yeyote anayehusika na vitisho hivyo kuacha mara moja.

"Unyanyasaji huu lazima ukomeshwe mara moja," alisema.

Machafuko yalizuka kati ya baadhi ya maafisa wa IEBC na wafuasi wa Azimio, baada ya ajenti mkuu wa Muungano huo Saitabao Kanchory kumtaka Chebukati kutotangaza matokeo.

Mzozo huo ulitokea baada ya Seneta Mteule wa Narok Ledama Olekina, wakala wa Raila Saitabao Ole Kanchory na Mbunge mteule wa Nyakach Aduma Owuor kumtaka Chebukati kutotangaza matokeo. 

Walikabiliwa na wanachama wa Kenya Kwanza wakitarajia tangazo la Chebukati.

Wawili hao waliokolewa na maafisa wa GSU waliotumwa Bomas of Kenya waliokuwa wakishika doria na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.