logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mmkubali rais mpya baada ya kesi ya kupinga matokeo, Atwoli awaambia Wakenya

Atwoli amewataka Wakenya kumkubali rais mpya baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu

image
na Samuel Maina

Uchaguzi20 August 2022 - 10:26

Muhtasari


  • •Atwoli ambaye ni mshirika wa muungano wa Azimio alisema watu hawafai kuangazia jambo moja kwani ni lazima tuendelee na kukuza nchi.
  • •Pia aliwataka wanaotumia mitandao ya kijamii kuwachochea wengine kuzua vurugu waache kwa sababu nchi haiko tayari kwa hali hiyo.
Bosi wa COTU Francis Atwoli

Katibu mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Francis Atwoli amewataka Wakenya kumkubali rais mpya baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu, kwa ajili ya amani.

Katika video iliyofikia Radio Jambo, Atwoli ambaye ni mshirika wa muungano wa Azimio alisema watu hawafai kuangazia jambo moja kwani ni lazima tuendelee na kukuza nchi.

“Jinsi tulivyomshauri Raila ni lazima tupitie njia ya kisheria na kusubiri uamuzi huo na hata Rais Mteule William Ruto alisema atakubali uamuzi wa mahakama,” akasema.

Pia aliwataka wanaotumia mitandao ya kijamii kuwachochea wengine kuzua vurugu waache kwa sababu nchi haiko tayari kwa hali hiyo.

"Iache mahakama ifanye kazi yake, na kabla ya hapo tudumishe amani. Wanaozungumzia vurugu waangalie nyuma wakati tunatafuta uhuru, mambo yalivyokuwa, hatuko tayari kurudi huko."

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga alisema atahamia Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya uchaguzi ambayo yalitangazwa Jumatatu Agosti 15.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati Jumatatu alimtangaza William Ruto kuwa rais mteule.

Ruto alipata kura 7,176,141 huku Raila akipata kura 6,942,930.

Raila alidai kuwa tangazo la Ruto kama rais mteule lilikuwa batili.

"Mtu yeyote asijichukulie sheria mkononi. Tunafuata njia za kikatiba na halali kubatilisha tamko la Chebukati haramu na kinyume na katiba. Tuna hakika kwamba haki itatendeka," alisema.

Sheria inaruhusu lalamiko katika Mahakama ya Juu wakati mgombeaji mmoja anahisi kutoridhika na matokeo ya uchaguzi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved