Chama cha Roots kinachoongozwa na wakili msomi George Wajackoyah kimemuandikia barua ya kulalamika aliyekuwa mgombea mwenza wa Wajackoyah, Justina Wamae kwa kile walisema Wamae aliwapongeza rais mteule William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua, kinyume na katiba ya chama.
Katika baria hiyo ambayo Wajackoyah alipakia Jumatatu kwenye ukurasa wake wa Twitter, miongoni mwa malalamishi mengi ni lile la kusema kwamba Wamae kwa mara kadhaa ameonekana kuenda kinyume na katiba ya chama hicho kwa kufanya mambo na maamuzi mengi kama yeye au kwa niaba ya chama cha Roots.
Wikendi iliyopita, Wamae kupitia Twitter yake aliandika jumbe kadhaa za kuwahongera Ruto na Gachagua huku akisema kwamab anaweza kubali uchaguzi huo uliokamilika uliandaliwa kwa njia nzuri na kusema kwamba Ruto na muungano wake waikuwa wamejipanga vilivyo kuliko chama chake cha Roots.
"Imenichukua siku 4 kusikiliza hoja kutoka kwa kura zote kuhusu iwapo IEBC ilikuwa huru, haki na uwazi na ninaweza kusema kwa ujasiri kwamba uchaguzi ulikuwa wa wazi kwa sababu mawakala wa vituo vya kupigia kura ambao ni wakuu katika mchakato huu wangekuwa,"
"Roots Party ambao kama mwanachama ninaweza kusema kwa ujasiri kwamba hatukuwa na mpangilio kuhusiana na uhamasishaji wa mawakala unaosema kuwa kura ziliibiwa ni upuuzi tu. Kama viongozi wajao, tunapaswa kuacha kuzikejeli taasisi zetu jambo ambalo litatafsiriwa kuwa ni uchochezi wa umma dhidi yake," Wamae aliandika kwenye Twitter, matamshi ambayo yamezua nyufa hata zaidi katika uongozi wa chama hicho.
Barua hiyo pia iliteta kwamba Wamae alimhongera Ruto kwa ushindi na kusema jambo hilo linaonesha kwamba amejitenga kabisa na chama cha Roots.
"Hongera H.E Ruto na H.E Rigathi kwa ushindi wenu. Kama mwakilishi wa vijana wa Kenya nitaunga mkono kwa vyovyote niwezavyo ili kufanikisha Kenya iliyo salama kifedha," Wamae aliandika.
Kutokana na mkanganyiko huu ambao Wamae anasemekana kuleta katika chama cha Roots, barua hiyo ilimtaka kujiwasilisha mbele ya jopo na haki na nidhamu ya chama hicho tarehe 26 Agosti ili kujibu malalamishi hayo.