Aliyekuwa jaji mkuu David Maraga amepuuzilia mbali ujumbe ambao umekuwa ukisambazxwa kwenye mitandao ya kijamii ukidai kuwa ni maneno yake ya kusema naibu rais William Ruto alishinda uchaguzi uliokamilika majuma mawili yaliyopita kwa njia halali.
Katika ujumbe huo ambao ni ghushi, unadai kwamba Maraga alisema Ruto alimshinda Raila kwa njia halali na bila tashwishi yoyote anafaa kuapishwa kuingia ikulu Agosti 30 kulingana na katiba.
Aidha, ujumbe huo pia unazidi kusema kwamba Maraga alidai amesikitishwa sana na hatua ya rais anayeondoka Uhuru Kenyatta kushinikiza mahakama ya upeo kubatilisha matokeo ya IEBC kwa kumpendelea Raila Odinga.
Ujumbe huo uliosambazwa pakubwa haswa kwenye mtandao wa Twitter na Facebook ulizua mjadala mkali huku baadhi wakiamini ni maneno ya Maraga na idadi kubwa ya Wakenya wakiamini ni ujumbe ghushi kwani mtu mwenye heshima zake na akili zake timamu kama Maraga hawezi kutoa matamshi kama hayo yanayolenga kuzua uhasama miongoni mwa wakenya haswa kipindi hiki ambacho hatima ya ushindi wa Ruto inasubiriwa kutolewa na jopo la majaji wa mahakama ya upeo katika muda wa siku 14 zijazo.
Hili lilimfikia Maraga kwa mshangao mkubwa ambapo kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter aliupuuzilia mbali na kusema hayo si maneno yake hata kidogo.
“Tweet hii inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidaiwa kuandikwa na mimi ni FEKI, tafadhali puuza,” Maraga aliandika.