logo

NOW ON AIR

Listen in Live

DP Ruto - Sakaja ni mgombea wa kimiujiza, ushindi wako haungewezekana bila Mungu

"Johnson Sakaja, wewe ni mgombea wa kimiujiza. Kuchaguliwa kwako kwa hakika ni muujiza na haingefanyika bila Mungu,” Rais Mteule William Ruto.

image
na Davis Ojiambo

Uchaguzi25 August 2022 - 10:26

Muhtasari


  • • Ruto alihudhuria kuapishwa kwa Sakaja na kuahidi kuachilia fedha za kaunti kwa muda unaostahili.
Rais mteule wa Kenya wakitabasamiana na gavana mteule wa Nairobi wakati wa kuapishwa kwake

Rais mteule William Ruto amemsifia vikali gavana mteule wa Nairobi Johnson Sakaja na kumuita mwaniaji wa kimiujiza aliyepata ushindi wake kwa njia ya kimiujiza mno.

Ruto ambaye alikuwa mmoja wa viongozi tajika waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Sakaja kama gavana katika ukumbi wa kimataifa wa KICC alisema kwamba Sakaja aliuheshimisha muungano wa Kenya Kwanza kwa kushinda ugavana Nairobi licha ya vita vikali kuhusu sakata lake la kumiliki shahada ya kwanza, ambacho kikatiba ndicho kigezo kikubwa cha mmoja kuruhusiwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEB kuwania ugavana katika jimbo lolote nchini Kenya.

Ruto ambaye anajulikana na wengi kwa kumkumbatia Mungu katika kila kitu hakusita kutaja kwamba ushindi wa Sakaja haungewezekana pasi na uwepo wa Mungu kutokana na pingamizi kali alizokabiliana nazo.

“Hongera kutoka kwa familia yangu na Kenya Kwanza. Umetuheshimisha pakubwa. Johnson Sakaja, wewe ni mgombea wa kimiujiza. Kuchaguliwa kwako kwa hakika ni muujiza na haingefanyika bila Mungu,” Rais Mteule William Ruto alisema wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Johnson Sakaja.

Kinara huyo wa chama cha UDA ambacho kilimpa tikiti Sakaja aliendelea mbele kutoa ahadi sufufu kwa marais hao wa kaunti na kuwaahidi kwamba serikali yake endapo ushindi wake utadumishwa na mahakama ya upeo, basi itakuwa inaachilia fedha za kufanikisha maendeleo katika ngazi za kaunti kwa wepesi na muda unaofaa, kinyume na serikali ya sasa ambayo inachelewesha fedha hizo na kulemaza shughuli muhimu katika ngazi za ugatuzi kaam vile hospitali na maji.

“Serikali ya Kenya Kwanza itatoa mapato yanayoweza kugawiwa kwa wakati ili tuweze kusimamia vyema nchi yetu na kuwawezesha magavana kutekeleza majukumu yao. Tunaunga mkono kaunti kukuza mapato ya kibinafsi," Ruto aliongeza.

Sakaja aliapishwa Alhamis kama gavana wa nne wa kaunti ya Nairobi baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ambapo alimbwaga mshindani wake wa karibu Polycarp Igathe aliyekuwa akiwania kupitia tikiti ya chama cha Jubilee.

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved