Rais mteule William Ruto ataapishwa Jumanne, Septemba 13, 2022.
Hii ni baada ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali ombi la mpinzani wake Raila Odinga, kutaka ushindi wa Ruto ubatilishwe.
Msururu wa shughuli utafanyika katika muda wa wiki moja ijayo kabla ya hafla ya kuapishwa kwa Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.
Kulingana na kifungu cha 141 cha Katiba ya Kenya rais mteule anafaa kuapishwa Jumanne ya kwanza baada ya siku saba za mahakama kutoa uamuzi.
Kuapishwa kwa rais mteule William Ruto kutafanyika Jumanne, Septemba 13.
Kisha Rais mteule atachukua madaraka kwa kula kiapo cha utii na kuapa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.
Wakati wa hafla hiyo Rais Mteule ataapishwa hadharani mbele ya Jaji Mkuu au Naibu Jaji Mkuu ikiwa Jaji mkuu hayupo.
Baada ya kuapishwa, Rais atatia saini cheti cha kuapishwa na Rais anayemaliza muda wake atamkabidhi Rais zana za mamlaka: upanga na Katiba.
Mahakama ya upeo siku ya Jumatatu ilithibitisha kuchaguliwa kwa William Ruto kama Rais wa tano wa Jamhuri ya Kenya. Akisoma uamuzi huo, Jaji Mkuu Martha Koome alisema Ruto alipata asilimia 50 pamoja na kura moja kama inavyohitajika kisheria.
Ruto alipata kura milioni 7.1 huku mpinzani wake wa karibu Raila Odinga akipata kura milioni 6.9.