Jamaa aliyejitambulisha kama Ronald Mulongo ,34, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Linet Wangila.
Ronald alisema mkewe alitoroka ndoa yao ya miaka minane mwaka jana baada ya kumshuku kuwa na mpango wa kando.
"Nilikuwa nafanya kwa kampuni. Hiyo kampuni kuna wamama na wazee. Mke wangu alipata naongea na mwanamke mmoja kwa simu. Kwa kweli alinipata, nilijaribu kumweleza hakuna kitu lakini hakunisikia," alisema.
Ronald alikiri kwamba wakati alipopatikana na mkewe ndio alikuwa anajaribu mahusiano na mwanamke huyo mwingine.
"Alikuwa ameniamini sana. Vile aliona hivyo alikasirika akaondoka. Wakati huo hakuonekana kuwa na hasira. Nilishangaa ata asubuhi aliamka akanipikia chai lakini jioni nikitoka kazini sikumpata," alisema.
Alieleza kuwa Bi Linet alirudi nyumbani kwao pamoja na watoto wao wawili.
Linet alipopigiwa simu alifichua kwamba aligura ndoa hiyo baada ya mienendo ya mumewe kuanza kubadilika ghafla.
"Ilifika mahali akaanza kubadilika. Ilifika mahali nikijaribu kumweleza kitu anaanza kuwa mkali. Niliona badala ya kusumbuana na yeye ni heri nimpatie nafasi," alisema.
Alibainisha kuwa tayari amemsamehe mzazi huyo mwenzake ila akatupilia mbali uwezekano wa wao kurudiana.
"Mimi nilikwambia nishakusamehe lakini hakuna nafasi nyingine. Ulinionyesha madharau, Ulinitusi, ukatukana wazazi wangu. Nimeachilia moyo wangu," alisema.
Mama huyo wa watoto wawili alifichua kwamba mumewe alimwambia tayari amesonga mbele na maisha yake na ameoa mwanamke mwingine.
Huku akijitetea, Ronald alisema alimwambia mkewe hayo kutokana na hasira.
"Hatukuwahi kuzinguana. Kosa moja lisifanye tuvunje boma yetu," Ronald alimwambia mkewe.
Linet alidokeza kwamba madharau ya mumewe dhidi yake yalianza baada ya yeye kumtafutia kazi jijini Nairobi.
Alisema mumewe alianza kumuonyesha madharau mengi kwa nyumba, kudhalilisha wazazi wake na hata kumpiga.
"Nimeishi na mume wangu miaka saba. Alipata kazi Nairobi. Mimi ndio nilimtafutia. Mzee wangu alibadilika. Alikuwa ananipiga, anatusi hadi mama yangu akisema ni mjinga na hawezi kumwambia kitu," alisema.
Aliongeza, "Jana amenipigia simu akaniambia anataka kuchukua kijana alafu msichana nijipange na yeye. Alitaka achukue mtoto mmoja kwa sababu kuna mwanamke ameoa na anataka wamlee pamoja."
Ronald hata hivyo alibainisha kwamba alikuwa akimtishia mkewe ili amshinikize kurudi nyumbani.
Linet alisema, "Nimempatia nafasi kwa muda mrefu. Nimekuwa mtu wa kuficha siri. Nilikuwa namwambia mamake masaibu napitia alafu anaenda kutangaza. Nimekuwa namlisha kama mtoto mdogo."
Alifichua kwamba aliwahi kumpata Ronald akizungumza na mwanamke mwingine kwa simu na hata akampatia simu azungumze naye.
"Nampata kwa kitanda akiongea na mwanamke. Alafu ananicheka akiniita mimi niongee na huyo mwanamke," alisema.