Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo Joseph Ogidi almaarufu Gidi amewakosoa watu mashuhuri ambao wanazozana kuhusu mavazi waliyovaa kwenye harusi ya Akothee siku ya Jumatatu, Aprili 10.
Akizungumza kwenye video aliyochapisha siku ya Alhamisi, mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la Gidi Gidi- Maji Maji alidai kuwa kuna baadhi ya mastaa walioalikwa ambao wamegeuza harusi hiyo kuwa vita vya aliyeshona vitenge vyao.
"Wahusika waliohudhuria harusi ya Akothee wamegeuza siku hii muhimu sana ya Akothee kuwa pambano kuhusu nani alishona kitenge cha nani, nani hakushonewa na vitu kama hivyo. Ni upuuzi gani huo?" Gidi alilalamika.
Mtangazaji huyo mahiri alibainisha kuwa ni aibu sana kwa watu kugeuza hafla muhimu kama hiyo kuwa vita vya nguo zilizovaliwa.
Alishangaa kwa nini mama huyo wa watoto watano ambaye alikuwa akifanya harusi yake ya pili aliwaalika watu kama hao kwenye hafla hiyo.
"Aibu kwenu wahusika kama hao. Wacheni kuharibia Akothee siku yake bana. Siku hiyo ilikuwa kuhusu Akothee, Omosh, na harusi. Sio mambo ya nani alishona kitenge, nani alishonewa, na mambo kama hayo," alisema.
Gidi alibainisha kuwa angealikwa kwenye harusi hiyo angevalia suti iliyofumwa vizuri bila kujigamba kuhusu nani aliyeitengeneza.
Akothee na mumewe Denis Shweizer 'Omosh' walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, Nairobi siku ya Jumatatu. Harusi hiyo ambayo ilikuwa ya pili ya mwimbaji huyo ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua 300 walikuwa wamealikwa kwenye hafla hiyo ya kufana.
Gidi hata hivyo hakuwa miongoni mwa wageni wengi mashuhuri ambao walihudhuria harusi hiyo ya kifahari kwani hakualikwa.
Siku chache zilizopita, mtangazaji huyo mahiri alikuwa ameibua malalamishi kwa Akothee kwa kutomualika kwenye hafla hiyo.
"Dada yangu Esther Akoth almaarufu Akothee. Wanakijiji wangu wa Kanyamwa wanauliza kwa nini hujanialika kwa harusi yako kubwa. Lazima tushuhudie ufugaji wa simba jike, kulundeng," Gidi alisema kwenye Facebook.
Pia alimtaka mume wa mwimbaji huyo, Denis Shweizer kumkumbuka yeye na wanakijiji wengine wakati wa kulipa mahari.